EAC YAITOLEA NJE SUDAN NA SOMALIA

Tuesday, December 4, 2012

NCHI wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC zimepinga uanachama wa Sudan Kusini na Somalia katika Jumuiya hiyo. Kamati ya mawaziri na wataalamu ya Jumuiya hiyo imekataa ombi la uanachama wa nchi hizo baada ya kuchunguza hali ya kiuchumi na kisiasa ya nchi mbili hizo. Juzi iliwasilisha rasmi ripoti yake kwa kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kilichofanyika wiki iliyopita mjini Nairobi Kenya. Wawakilishi wa nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Tanzania na Kenya ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walianza kujadili maombi ya kujiunga na jumuiya hiyo ya nchi za Sudan Kusini na Somalia tarehe 19 Novemba. Sudan Kusini ilijitenga na Sudan tarehe 9 Julai mwaka uliopita. Kwa mujibu wa wataalamu wa EAC nchi hiyo bado inakabiliwa na matatizo ya kisiasa na wala uchumi wake ambao asilimia 98 yake inategemea mauzo ya mafuta si wa kuridhisha. Licha ya kuwa nchi hiyo sasa inamiliki asilimia 75 ya mafuta yote ya Sudan mbili lakini bado inategemea ardhi ya Sudan ili kusafirisha mafuta yake kuelekea masoko ya kimataifa. Hii ni mbali na kuwa vituo vyote va usafishaji mafuta hayo vinapatikana katika ardhi ya Sudan. Mzozo kuhusiana na umiliki wa eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Abyei ambalo liko kwenye mpaka wa pamoja wa nchi hizo ni jambo lililozipelekea kukaribia kupigana mwezi Aprili uliopita. Vita hivyo viliepukwa kufuatia upatanishi wa Umoja wa Afrika uliongozwa na Thabo Mbeki, rais wa zamani wa Afrika Kusini, na hatimaye kutiwa saini mkataba wa amani mjini Kampala. Licha ya nchi mbili hizo kutia saini mkataba huo lakini bado zinagombana kuhusiana na umiliki wa Abyei. Maandamano yaliyofanywa hivi karibuni na wananchi wa Sudan dhidi ya pendekezo la Umoja wa Afrika kuhusu Abyei ni dalili ya wazi inayothibitisha suala hilo. Mbali na pato dogo hilo la mafuta, Sudan Kusini inanufaika na sehemu ndogo sana ya asilimia 4 ya kilimo kutokana na kuwa asilimia 35 ya ardhi ya nchi hiyo imefunikwa kuwa na misitu. Kwa msingi huo ni masuala mawili hayo ya kutokuwepo usalama wa kutosha na udhaifu wa kiuchuni ndiyo yameipelekea nchi hiyo kutokubaliwa kuwa mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

0 comments:

Post a Comment