Dowans yawabwaga wanaharakati mahakamani

Wednesday, September 7, 2011


WAMILIKI wa Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans jana walitoka mahakamani kwa furaha baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutupilia mbali pingamizi la wanaharakati waliofungua kesi kupinga tuzo yake ya Sh94 bilioni.

Kutokana na uamuzi huo, sasa Dowans imevuka kizingiti cha kwanza na imebakiwa na cha pili cha pingamizi la Serikali na ikishinda njia itakuwa nyeupe kulipwa fidia ya mabilioni hayo ya fedha inazodai kutokana na kuvunjiwa kwa mkataba wake kinyume cha utaratibu.

Dowans kupitia kwa wakili wake, Kennedy Fungamtama iliwawekea pingamizi wanaharakati waliokuwa wakipinga usajili wa tuzo na malipo yake ya fidia ya Sh94bilioni kutoka Shirika la Umeme (Tanesco).

Wanaharakati hao ambao walidai kuwa wameamua kupinga usajili wa tuzo hiyo kwa maslahi ya umma ni pamoja na Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC). Wengine ni Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT) na Kampuni ya Sikika (Sikika Company Limited- CL). Taasisi hizo ziliwakilishwa na wakili, Dk Sengondo Mvungi, pamoja na Mwanahabari Timothy Kahoho.

Katika pingamizi lake, Wakili wa Dowans, Fungamtama pamoja na mambo mengine, alidai kuwa wanaharakati hao hawana haki ya kisheria ya kuingilia suala hilo kwa kuwa hawakuwa wahusika katika mgogoro huo.

Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo jana, Jaji Emilian Mushi alikubaliana na pingamizi la Dowans kuwa wanaharakati hao hawana haki ya kisheria kuingilia katika suala hilo.

Hivyo, Jaji Mushi aliwaondoa wanaharakati hao katika shauri hilo na kwa uamuzi huo, pingamizi la wanaharakati hao kuzuia usajili wa tuzo ya Dowans yametupiliwa mbali moja kwa moja.

Badala yake, shauri hilo sasa linabaki dhidi ya Dowans na Tanesco ambao pia wanapinga usajili wa tuzo hiyo.

Baada ya kuwaengua wanaharakati hao katika shauri hilo, Jaji Mushi alisema kwa sasa anaendelea kuandika uamuzi baina ya Dowans na Tanesco na kwamba atautoa muda si mrefu.

Uamuzi huo baina ya Dowans na Tanesco ndiyo utakaotoa hatima ya sakata hilo. Kama mahakama itakubaliana na maombi ya Dowans basi tuzo hiyo itasajiliwa na kuipa nguvu ya kisheria kulipwa mabilioni hayo. Lakini kama mahakama itakubaliana na pingamizi la Tanesco, basi tuzo haitasajiliwa na hivyo Dowans haitaweza kulipwa fidia hiyo.

Katika uamuzi wake jana, Jaji Mushi alikubaliana na hoja za wakili Fungamtama wa Dowans kuwa kwanza wanaharakati hao hawakutimiza matakwa ya kisheria pamoja na kanuni zinazotumika katika mashauri ya uwakilishi mahakamani.

Jaji Mushi alisema wanaharakati hao kwanza hawakuambatanisha vielelezo mbalimbali vinavyohusika katika shauri hilo ikiwamo tuzo ya ICC kwa Dowans kama Kanuni ya Nane ya Usuluhishi sura ya 15 inavyoeleza.

“Inatosha kusema kwamba kutimiza masharti ya kanuni ya Nane ni jambo la lazima. Hii ni kusema kwamba kuonyesha au kuwasilisha tuzo katika maombi ni jambo la muhimu kuonyesha mahakama ina nguvu ya kisheria kufanya ilichoombwa kukifanya,” alisema Jaji Mushi katika uamuzi wake huo huku akirejea katika kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa kuhusiana na hoja hizo.

Pia Jaji alikubaliana na hoja ya Fungamtama kuwa katika kuwasilisha maombi mahakamani, kibali cha mahakama ni cha lazima kama inavyoelezwa katika Amri ya Kwanza ya Kanuni ya 8(1) ya Mwenendo wa Mashauri Madai.

Kuhusu madai ya wanaharakati kuwa wameamua kuingilia katika suala hilo kwa maslahi ya umma, Jaji Mushi alikataa hoja hizo na kukubaliana na hoja za Wakili Fungamtama kuwa maslahi ya umma yanalindwa na kutetewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Dk Mvungi katika hoja hiyo alidai kuwa ingawa inakubalika kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiye mlinzi wa maslahi na haki za umma lakini haina maana kwamba watu wengine katika jamii hawana haki ya kisheria kwa kuwa AG anasimama kwa niaba yao.

Lakini Jaji Mushi alikataa maelezo hayo ya Dk Mvungi na kukubaliana na hoja za Wakili Fungamtama akisema kuwa kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 30 (1) (e) cha Sheria ya Usuluhishi, maslahi na haki za umma hulindwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Huku akirejea kesi mbalimbali, Jaji Mushi alisema mahakama inakubali kuwa kanuni zinazoongoza nchini kama ilivyo katika nchi nyingine duniani zinazoongozwa na sheria maslahi na haki za umma hulindwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tu.

“Hivyo wanaodai hawana haki ya kudai jambo lililo ndani ya uwezo wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwa taarifa, naomba niwaeleze wadai kuwa wadai wa tatu (Tanesco) kwa kutokuridhishwa na tuzo ya ICC nao wamewasilisha maombi katika mahakama hii wakipinga uhalali wa tuzo hiyo,” alisema Jaji Mushi.

Alisisitiza kuwa ni kwa kutambua hilo ndiyo maana katika maombi hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameungana na wanasheria wa Tanesco kuiwakilisha Tanesco.

“Hivyo nimeridhika kuwa wadai hawakufanikiwa kuonyesha kwamba wana haki au maslahi… Kwa hiyo maombi yote yanafutwa na waombaji watabeba gharama za kesi,” alisema Jaji Mushi.

Novemba 15, mwaka jana Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), chini ya Mwenyekiti wake, Gerald Aksen na wasuluhishi Swithin Munyantwali, Jonathan Parker, iliiamuru Tanesco iilipe Dowans fidia ya Sh94 bilioni kwa kuvunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Kutokana na uamuzi huo, Januari 25 mwaka huu Dowans iliwasilisha katika Mahakama Kuu maombi ya usajili wa tuzo yake hiyo kupitia kwa wakili Fungamtama, ili ulipwaji wa fidia yake hiyo ufanyike kisheria.

0 comments:

Post a Comment