BANK-MOON AIONYE ISRAEL

Tuesday, December 4, 2012

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, ameonya kuhusu mpango wa Israeli kuhusiana na ujenzi wa makao mapya ya walowezi kwa kuhofia athari za upotevu wa amani. Ki-moon ameonyesha hali ya wasiwasi juu ya ujenzi ya huo na kusisitiza kuwa ujenzi huo usitishwe katika eneo hilo kwa kuwa endapo ujenzi huo utaendelea unaweza kuvuruga hali ya amani. “Mpango wowote wa kujenga makazi katika sehemu inayojulikana kama E1 ni lazima usitishwe kwa kuwa hatua hiyo itakuwa ni pigo kubwa katika fursa iliyopo ya mazungumzo ya amani,” alisema. Naye Mkuu wa sera katika Muungano wa Ulaya, Catherene Ashton, alielezea wasiwasi kuhusu mpango wa ujenzi wa makazi mengine ya walowezi na kuwataka kuachana na mpango wa ujenzi huo . Kauli hiyo imetolewa mara baada ya Israeli kusema mpango wao wa kuongeza nyumba elfu tatu kwa makazi yaliopo na inatarajia kuongeza makazi mapya kwa kuunganisha yale yaliyopo katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalemu Mashariki. Israeli Ilitangaza mpango huo kufuatia kura ambayo iliyopigwa na Umoja wa Mataifa (UN) iliyoipandisha Palestina hadhi kuwa dola mwangalizi katika umoja huo. Kutokana na hali hiyo, Kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas alipokewa kwa shangwe mjini Ramallah katika ukingo wa Magharibi aliporudi nyumbani kutoka kwenye mkutano huo ambao uliipa sifa taifa hilo kwa kupandishwa hadhi. Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameahidi kuendelea na mpango wake wa ujenzi licha ya kuwepo kwa sintofahamu juu ya ujenzi huo.

0 comments:

Post a Comment