Serikali yaruhusu wafanyabiashara kuagiza sukari nje

Wednesday, September 7, 2011


SERIKALI itatoa leseni kwa wafanyabiashara wa hapa nchini, ili kuwawezesha kuagiza tani 120,000 za sukari kutoka nje ya nchi na sukari hiyo haitalipiwa kodi, ukiwa ni mkakati wa kukabiliana na upungufu wa bidhaa hiyo.

Chini ya mkakati huyo, Bodi ya Sukari Tanzania, hivi karibuni itatangaza kupitia vyombo vya habari namna , kampuni zinavyotakiwa kuomba leseni hizo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mohamed Muya, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa uamuzi huo ulifikiwa katika kikao kilichofanyika juzi.Alisema kikao hicho kiliwashirikiosha Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Cyril Chami na maofisa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Fedha na Uchumi.

“ Katika mkutano huo tulikubaliana kuwa kila kampuni itaruhusiwa kuagiza tani 5,000 za sukari ili kutoa nafasi kwa kampuni nyingi zaidi kuagiza bidhaa hiyo,” alisema Muya.Alisema serikali itawafuatilia kwa karibu wafanyabiashara watakaopewa leseni ya kuagiza sukari, ili kuhakikisha kwamba bidhaa hiyo inapatikana kwa bei iliyokubaliwa ambayo ni chini ya wastani wa Sh 2,000 kwa kilo.

“ Tutafuatilia kwa karibu hadi kwenye maghala ili kuhakikisha kuwa kampuni hizo kweli zimeagiza sukari kutoka nje, pia tutafuatilia kuona kwamba sukari hiyo haivushwi kwenda kuuzwa katika nchi za Kenya na Uganda,” alisema.Katibu mkuu huyo alisema kampuni zitakazokiuka kanuni za bodi za uagizaji nje bidhaa, zitakabiliwa na faini ya Sh 30 milioni au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Muya alisema kampuni hizo pia zitaruhusiwa kuagiza sukari kutoka katika nchi yoyote ambazo zitaona ni rahisi kuagiza.Alisema ili sukari kutoka nje iweze kuwafikia watumiaji, wananchi watatakiwa kuvumilia kwa zaidi ya miezi mitatu ndipo itakuwa imewasili nchini na kusambazwa.

“ Ndani ya mwezi mmoja tutakuwa kwenye mchakato wa kutangaza na kuteua kampuni hizo za kuagiza sukari, katika kipindi cha miezi miwili watakuwa wameagiza na kuifikisha nchini,” alisema Muya.

Bei ya sukari katika nchi za Kenya na Uganda
Katibu mkuu huyo alisema katika nchi ya Kenya, bei ya sukari inauzwa kwa Sh4,000 kwa kilo wakati Uganda inauzwa kwa Sh3,500 ikilinganishwa na fedha za Tanzania.

“ Ndiyo maana kuna upungufu wa bidhaa hiyo hapa nchini na sababu kubwa inatokana na wafanyabishara wasiokuwa waaminifu kuiuza nje ya nchi kwa lengo la kujipatia faida zaidi bila kupata vibali kutoka kwenye bodi,” alisema Muya.

Alisema hata hivyo serikali itaimarisha ulinzi kwenye mipaka ili kukabiliana na uvushaji wa sukari nje ya nchi kwa kutumia njia za Panya.

“ Bei kubwa ya sukari katika nchi za Kenya na Uganda imekuwa kichocheo cha wafanyabishara kusafirisha bidhaa hiyo kwa magendo ili kujitajirisha,” alisema Muya.

Katibu Mkuu huyo pia alisema serikali itaunda kikosi kazi cha wataalamu watakaofanya utafiti wa taratibu za soko la sukari na ukokotoaji wa bei ili kuishauri juu ya hatua za kuchukua kukabiliana na changamoto zilizopo.

0 comments:

Post a Comment