BALOZI wa Palestina hapa nchini, Dk Nasri Abujaish amesema ushindi iliyoupata nchi yake baada ya kupigiwa kura na hatimaye kuipandisha hadhi ni ushindi wa dunia nzima katika kupigania haki za binadamu, uhuru na amani. Dk Abujaish aliyasema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za ubalozi huo, zilizopo Upanga ,jijini Dar es Salaam. “Huu ni ushindi wa dunia nzima kwa ajili ya haki za binadamu, uhuru, utaifa na amani. Kwa hili ulimwengu useme sasa ‘yatosha kwa utawala na ukandamizaji’,” alisema Dk Abujaish. Hivi karibuni Baraza la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa kauli moja kwa wingi wa kura, kupandisha hadhi ya eneo la Palestina baada ya nchi 138 kuunga mkono hatua ya kuitambua Palestina kuwa nchi ambayo si mwanachama wa Umoja wa Mataifa lakini itaruhusiwa kushiriki katika shughuli za umoja huo. Hata hivyo mataifa tisa yakijumuisha Israel na Marekani yalipiga kura ya kupinga mpango huo, huku mataifa 41 yakisusia shughuli hiyo. Kura hiyo yenye umuhimu mkubwa, sasa inaiwezesha Palestina kuwa na ushirika katika Umoja wa Mataifa na mashirika mengine kama vile Mahakama ya ICC. Alisema baada ya hatua hiyo, Palestina itakuwa na uwezo wa kuzitumia mamlaka za Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita na inaweza kuishtaki Israel kutokana na vitendo vyake vilivyo kinyume cha haki za binadamu. Alisema chini ya hatua hiyo, wafungwa wa kisiasa watakuwa wakichukuliwa kama wafungwa wa vita chini ya Azimio la nne la Geneva. “Kutokana na ushindi huo, uvamizi wa Israel unakuwa umekataliwa na Taifa la Palestina limeshinda. Tunatumai kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakubali ombi la Palestina lililowasilishwa mwaka 2011 la kuipa uanachama wa moja kwa moja na kufikia mwafaka wa mipaka ya nchi mbili ulioanza tangu mwaka 1967,” alisema. Alisema ushindi huo pia utawawezesha kutafuta suluhisho kati yake na Israel kuhusu matamko yaliyokiuka sheria, Mji wa Jerusalem, mipaka, wakimbizi maji na rasilimali nyinginezo. “Nazishukuru nchi 138 zilizoipigia kura Palestina, zinatoka Afrika, Asia, Marekani Kusini na sehemu ya Ulaya. Kwa kipekee kabisa tunaishukuru Tanzania kwa kusimama upande wetu. Kwa mara nyingine imeonyesha mshikamano wa kihistoria uliokuwepo,” alisema. Kuhusu mataifa yaliyopiunga mpango huo, Dk Abujaish alisema yanakwenda kinyume na kanuni za haki za binadamu zinazodai kuzipigania. Kwa muda mrefu sasa, Palestina imekuwa ikishinikiza kutambuliwa kuwa ni taifa huru, lakini imekuwa ikipata vipingamizi kutoka Marekani na washirika wake ikiwamo Israeli. Hata hivyo kiongozi wa palestina Mahamood Abbas, ameapa kuendelea na jiotihada za kuushinikiza Umoja wa Mataifa na mataifa mengine duniani, ili yakubali kuitambua Palestina. Nchi hiyo imekuwa ikipinga vikali utawala wa mabavu wa Israel ambayo imekuwa ikikalia baadhi ya maeneo yake, jambo linalosababisha kukua kwa mgogoro wa mara kwa mara. Hata hivyo mataifa mbalimbali duniani yamekuwa yakihimiza amani.
Popular Posts
-
NEW YORK, Marekani VIDEO iliyoonyweshwa mwishoni mwa wiki katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ambayo ilielezea madhara ya taratibu ana...
-
RAIS Jakaya Kikwete ameeleza mikakati ya Serikali yake kuwa ni kuhakikisha inamaliza kabisa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ifikapo...
-
Uingereza imesitisha kwa muda msaada iliyokuwa iipe Rwanda kwa sababu ya wasiwasi kuhusu kuhusika kwa nchi hiyo katika mzozo uliopo Jam...
-
Huduma ya Maji na Nishati (EWURA), Mhandisi Godwin Samwel, akizungumza na wanahabari jana jijini, Dar es Salaam kuhusu kupanda kwa bei za m...
-
KAMPUNI ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti imetoa msaada wa kilo 200 ...
-
HERIETH MAKWETTA MSANII wa muziki wa kizazi kipya kutoka Tanzania, Rehema Chalamila maarufu kama Ray C, yupo katika kituo maalumu cha msa...
-
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewasafisha aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Ofisa Utawala wa ubalozi ...
-
UPELELEZI wa kesi inayomkabili Msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya mauaji katika Maha...
-
Wananchi wameshauriwa kutekeleza agizo la Utalii kwa wote kwa kuyatembelea maeneo mbali mbali ya utalii Zanzibar ili kufahamu historia y...
-
KUTOKANA na kile kichoonekana ni kutaka kukabiliana na uhaba wa sukari na kupanda kwa bei yake, Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatarajia kukuta...
Habari Leo Tanzania, Media, (East Africa)
0 comments:
Post a Comment