TANZANIA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA VVU HADI KUFIKI 2015

Sunday, December 2, 2012

RAIS Jakaya Kikwete ameeleza mikakati ya Serikali yake kuwa ni kuhakikisha inamaliza kabisa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ifikapo mwaka 2015. Akilihutubia taifa kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani Rais Kikwete alisema: “Tunataka tupunguze maambukizi na ikiwezekana mpaka 2015, kuwe na maambukizi sifuri kabisa. Huu mradi tumeshauanza, ila leo ni kama tunauzindua upya.” Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa mkoani Lindi, Kikwete alitaja mikakati mbalimbali aliyosema Watanzania hawana budi kuifuata ili kufikia kwenye hatua hiyo. Miongoni mwa miakakati hiyo ni kuhamasisha watu kupima, waathirika kutumia Dawa za Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARV), kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, elimu ya Ukimwi kutolewa shuleni na kwamba Serikali yake itahakikisha waathirika wanapata dawa bila malipo. Alisema kwamba Serikali itahakikisha inaliingiza somo la kujikinga na Ukimwi katika mitalaa ya elimu nchini na kuongeza kuwa atatafuta fedha, ili kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa watoto hao. Rais Kikwete alifafanua kuwa katika mpango huo wa kutoa elimu ya Ukimwi kwa wanafunzi, Serikali imeweza kuwafikia asilimia 65 ya wanafunzi wa shule za msingi na asilimia 75 wa shule za sekondari. “Wapo wanaosema tunawafundisha watoto tabia mbaya, lakini hao wanaosema hivyo, ndiyo wamekuwa vinara wa kuwapeleka watoto wao Jando na Unyago,” alisema na kuongeza: “Mangariba wanatakiwa kuwapa watoto hawa elimu juu ya Ukimwi, jinsi ugonjwa huu unavyoambukizwa na jinsi ya kujikinga.” Aliwataka pia wazazi kutoona aibu kuwafundisha watoto wao jinsi ugonjwa huo unavyoambukizwa na kwamba wakifanya hivyo watakua wameokoa vifo na kumaliza maambukizi mapya. Kikwete alisema pia kwamba kuna mradi wa kutokomeza maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, ambapo aliwataka wajawazito kupima afya zao ili waweze kupewa ushauri wa jinsi ya kumkinga motto ili azaliwe bila kuwa na maambukizi. Alitaja jambo jingine muhimu kuwa ni kuwahimiza Watanzania kupima afya zao kwa hiari na kwamba hadi sasa watu 17 milioni nchini wameshapima.

0 comments:

Post a Comment