REBECCA BALIRA, Mtanzania anayeishi Uingereza, amehukumiwa kifungo cha miezi sita JELA na kumlipa msichana Methodia Mathias (21) fidia ya Pauni 3,000 (sh. Milioni 7.8) kwa kumtumikisha msichana huyo, ambaye ni Mtanzania mwenzake, kazi za kitumwa nyumbani kwake.
Balira (45) ambaye ni mtafiti wa masuala ya virusi vya Ukimwi (VVU) alitiwa hatiani na mahakama moja ya Southward, kusini mwa jiji la London, kwa kumweka Mathias nyumbani kwake kama mtumwa.
Msichana huyo alidai Balira alimpeleka Uingereza kutoka Tanzania, lakini akawa anamfanyia manyanyaso kibao ikiwa ni pamoja na kumtumikisha kazi nzito na kumshambulia kimwili.
Mahakama hiyo ilisikia jinsi rafiki wa Mathias, aitwaye Beatrice Kosgei, alivyopeleka malalamiko ya mwenzake kwenye taasisi ya Kalayaan ambayo huwasaidia wahamiaji wanaofanya kazi za majumbani mwa watu.
Ofisa kutoka taasisi hiyo aitwaye Kate Roberts alielezea masikitiko kwa vitendo ambavyo hufanyiwa wafanyakazi hao na kwamba hatua za kuwalinda zizidi kuimarishwa.
Mwendesha mashitaka, Caroline Haughey, alisema Balira aliweka mazingira ambayo yalionyesha wazi kumfanya msichana huyo awe utumwa.
Hata hivyo, mwanamke huyo alifutiwa mashitaka ya kuendesha biashara ya kuingiza watu Uingereza kwa ajili ya kuwanyonya na kuwadhalilisha.
0 comments:
Post a Comment