Serikali yamwongezea muda Mkurugenzi MCL

Saturday, September 17, 2011


MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Sam Shollei, amelipongeza gazeti la The Citizen kwa kutimiza miaka saba tangu kuanzishwa kwake na kusema kuwa, anayo furaha ya kuongezewa muda wa kufanya kazi nchini hadi mwakani.

MCL inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.Akizungumza kwenye sherehe fupi ya kupongeza gazeti hilo na uongozi wake jana, Shollei alisema ameongezewa kibali cha kuendelea kufanya kazi nchini kwa miezi sita zaidi na kwamba, anaipongeza Serikali kwa hatua hiyo ambayo ni njema kwa mustakabali wa Tanzania na Afrika Mashariki.

"Nimefurahi sana kuwa nanyi tena kwa siku ya leo, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa kutimiza miaka saba leo hii, hali iliyotokana na uchapakazi wenu uliotukuka, pia naomba niwaelezeni kwamba Serikali ya Tanzania imeniruhusu kuendelea kufanya kazi nchini kwa miezi sita mingine, naipongeza kwa hatua yake hiyo," alisema.

Shollei alizungumza hayo jana ikiwa ni miezi mitatu tangu Juni 15, kibali chake kiishe na Serikali kuendelea kukifanyia kazi kwa taratibu na hatimaye kumuongezea miezi sita.

Kuhusu hatua ambayo MCL imepiga, Shollei alisema ni kutoa mafunzo ya kitaalamu ya uandishi wa habari na mawasiliano kwa vijana wa Tanzania wanaohitimu vyuo vikuu kwenda Nairobi kujifunza kwa mwaka mmoja, kwa wastani wa vijana wanane kila mwaka na sasa wamehitimu vijana 33.

Alisema mkakati huo unaendelea na vijana hao wanapohitimu mafunzo yao wamekuwa wakirejea nchini kufanya kazi na Kampuni ya MCL, pia vyombo vingine vya habari vilivyopo nchini.

Alitaja mafanikio mengine kuwa, ni kampuni kufanya vizuri kwa magazeti yake inayochapisha, kwani hivi sasa gazeti la Mwananchi linatawala soko kwa asilimia 48, wakati Mwanaspoti likiwa na asilimia 45, huku The Citizen likishika soko kwa asilimia 28.

"Mwanaspoti linashika nafasi ya pili kwa kuuzwa nakala nyingi Mombasa, nchini Kenya kwa magazeti ya Kiswahili, sasa linauzwa maradufu ya gazeti jingine la Taifa Leo na Oktoba 15, mwaka huu litazinduliwa na kuanza kuuzwa jijini Nairobi, baadaye magharibi kwa Kenya na ndani ya miezi mitatu tuna uhakika litakuwa la pili kwa kuuza nakala nyingi nchini Kenya," alisema.

Alisema MCL imeajiri wafanyakazi 308 kwa mikataba ya aina mbalimbali, kati yao wanane ndiyo wataalamu kutoka Kenya, Zimbabwe na India, waliobaki ni Watanzania.

0 comments:

Post a Comment