BAADA ya juzi Jeshi la Polisi kuwahoji na kuwaachulia huru wabunge wa Chadema, jana asubuhi walikamatwa na kutupwa korokoroni hadi kesho watapokafikishwa mahakamani kujubu tuhuma za kumfanyia vurugu Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario.Wabunge wawili wa Chadema watakaofikishwa mahakamani kesho ni Sylivester Kasulumbai wa Maswa Mashariki na Susan Kiwanga (Viti-Maalum) pamoja na mkada wa chama hicho, Anuary Kashaga. waliwekwa rumande jana hadi Jumatatu
Wabunge hao jana waliitwa tena polisi na kuhojiwa kisha kuswekwa rumande mbele ya mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu.
Walifikishwa katika kituo cha polisi Igunga saa 3:15 na walihojiwa kwa saa nne. Baadaye Lissu alitoka na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa polisi imewashikilia kutokana na malalamiko yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya kuwa alipigwa na wabunge hao.
Lissu alisema Jeshi la Polisi limesema linawashikilia wabunge hao na likiendelea kuwasaka watu wengine ambao walihusika katika tukio hilo lililotokea Septemba 14 mwaka huu katika Kata ya Isakamaliwa, wilayani Igunga.
Kwa mujibu wa Lissu, polisi wamesema kuwa mkuu huyo wa wilaya amelalaka kuwa alivuliwa hijabu, viatu na kukatiwa mkufu ambao thamani yake haijajulikana pamoja na kupotelewa simu yake ya mkononi aina ya Sumsung, yenye thamani ya Sh400,000
“Polisi wamepuuza kabisa madai ya Chadema, lakini bahati nzuri kuna maadili, na kwa kuwa wamesema watawashikilia, mimi nawataka wawapeleke mahakamani tukutane huko Jumamatu (kesho),”alisema Lissu.
Hata hivyo, Lissu alisema hizo ni njama za kuipunguza nguvu Chadema katika uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 3, mwaka huu.
Ulinzi mkali kituoni
Polisi wilayani Igunga, jana iliimarisha ulinzi katika kituo chake cha Igunga ambako wabunge wa Chadema na mfuasi mmoja wa chama hicho wafikishwa na kuwekwa rumande kwa tuhuma za kumfanyia fujo mkuu wa wilaya hiyo.
Askari wenye silaha walionekana wakikizunguka katika kituo hicho huku gari la maji ya kuwasha likiwa tayari wakati wote zikitokea vurugu.
Askari hao waliokuwa wameshika bunduki, ngao na virungu, walikuwa wakizunguka kituo hicho na kufunga barabara zinazoingiana kutoka kituoni hapo.
Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Tahimini (Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai), Naibu Kamishna wa Polisi, Issaya Mungulu, alithibitisha polisi kuwashikilia wabunge hao na kueleza kuwa hatua nyingine ikiwamo dhamana zitafuata baadaye.
DC: Niliwekwa chini ya ulinzi kama mfungwa
DC Kimario hadharani
Mkuu wa Wilaya ya Igunga(DC), Fatma Kimario jana alijitokeza kwa mara ya kwanza hadharani na kusimulia mkasa wa kutekwa nyara na wafuasi wa Chadema akisema: "Waliniweka chini ya ulinzi kama mfungwa."
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ndiye mwakilishi wa Rais katika wilaya hiyo, alidai kuwa mbali na kumweka chini ya ulinzi, walimtukana matusi ya nguoni na kumdhalilisha.
“Waliingia na kunikuta nimekaa kwenye kiti walikuwa hawanifahamu mmoja akauliza DC yuko wapi. Yule mbunge akasimama kwenye meza kunitukana matusi mazito,” alidai DC Kimario.
DC huyo amefafanua baada ya kumporomoshea matusi hayo, Mbunge huyo alianza kumvuta kwa lengo la kumtoa nje ambapo hijabu aliyokuwa amevaa, ilitoka huku mbunge akimpandisha blaus hadi tumbo likaonekana.
“Lengo lao hasa walikuwa wanataka nikamsalimie Dk Slaa (Willibrod ambaye ni Katibu Mkuu Chadema). Kwa sababu wao walikuwa wengi sikuwakatalia, ilibidi nikubali, nikaenda hadi kwenye mkutano,” alisema.
Kimario ambaye kwa wadhifa wake pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, alisema siku hiyo, Chadema walipaswa kufanya mkutano wao eneo hilo saa 4:00 asubuhi hadi 6:00 mchana.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, siku hiyo yeye alikuwa na kikao na viongozi wa serikali ya Kijiji cha Isakamaliwa ambacho kilianza saa 8:00 hadi saa 8:45 mchana na wakati wanamvamia tayari kikao kilishamalizika.
“Kwenye kikao changu hakuna hata mjumbe mmoja wa Serikali alikuwa amevalia sare za CCM wala alama yoyote ya CCM… Kwa hiyo mkutano wangu ulikuwa wa kiserikali,” alisisitiza Kimario.
Alizitaja agenda za kikao chake hicho kuwa zilikuwa ni pamoja na kuzungumzia kamati za wafugaji, masuala ya elimu, mipaka ya taasisi za Serikali na wananchi na ujenzi wa nyumba bora na vyoo.
Pia alitumia mkutano huo na viongozi hao wa serikali ya kijiji hicho kuwatahadharisha warejeshe mfumo wa kila mgeni kutakiwa kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji kutokana na ongezeko kubwa la watu na uhalifu.
“Lile suala kwamba, nilikuwa nafanya uhamasishaji kwa CCM ni wongo mkubwa na hapakuwa na jambo lolote linalohusiana na uhamasishaji wa uchaguzi, au kupiga kampeni kwa CCM,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
0 comments:
Post a Comment