MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewasafisha aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 Milioni. Kutokana na uamuzi huo, Profesa Mahalu amesema anamshukuru Mungu akisema, yaliyotokana ni kwa sababu Mungu amempenda. “Mungu amenipigania sana na haki imetendeka, sasa hivi nakwenda kanisani kumshukuru Mungu, nanyi nawaambieni mkasome Zaburi 17,” alisema Profesa Mahalu kwa furaha na kukumbatiana na mawakili na ndugu zake. Profesa Mahalu na Martin walikuwa wakikabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya kula njama na kuiibia Serikali na kuisababishia hasara ya Euro 2,065,827.60, katika mchakato wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Hata hivyo, jana Mahakama hiyo iliwaachia huru ikisema kuwa upande wa mashtaka katika kesi hiyo namba 1 ya mwaka 2007, umeshindwa kuthibitisha mashtaka hayo bila kuacha mashaka. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ilvin Mugeta aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisema kuwa katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wote saba wa upande wa mashtaka, hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaowatia hatiani washtakiwa hao. Alisema ushahidi uliopo ni wa mazingira tu ambao ulikuwa umesimamia katika nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kuhusiana na mchakato wa ununuzi wa jengo hilo. Katika hukumu yake, Hakimu Mugeta alirejea na kusisitiza ushahidi uliotolewa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akimtetea Profesa Mahalu kuwa ni msomi mzuri, mchapakazi, mwadilifu na mwaminifu. Pia hakimu Mugeta alihoji ilikuwaje hata mshtakiwa wa pili, Martin akaunganishwa katika kesi hiyo kwa kuwa nyaraka zote zilizowasilishwa mahakamani hapo ambazo ndizo upande wa mashtaka ulizitumia katika mashtaka zilikuwa zinamhusisha mshtakiwa wa kwanza tu. “Mwishowe napenda kusema kwamba nimeshindwa kufahamu ni kwa nini mshtakiwa wa pili alishtakiwa na ndiyo maana katika hukumu hii sikugusia ushahidi wake wa utetezi,” alisema Hakimu Mugeta na kuongeza: “Kwa kuhitimisha ninasema kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka bila mashaka yote katika makosa yote sita na washtakiwa wote wanaachiwa huru katika makosa yote.” Wakati akisoma hukumu hiyo,Hakimu Mugeta alianza kuchambua ushahidi wa upande wa mashtaka na ushahidi wa utetezi kisha akaanza kuainisha ushahidi huo jinsi ulivyoweza au ulivyoshindwa kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa kosa moja baada ya lingine. Kwanza, Hakimu Mugeta alisema anawaachia huru katika kosa la pili la wizi na kwa sababu hiyo hata kosa la kwanza la kula njama ili kutenda kosa hilo likawa limekufa kwa kuwa makosa hayo yote yanategemeana. Akizungumzia kosa la kula njama, Hakimu Mugeta alisema dhana ya kosa hilo upande wa mashtaka uliegemea kwenye uwepo wa mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo. “Siko tayari kutumia dhana yao hiyo isipokuwa kama nitashawishiwa kupita mashaka yote kwamba matumizi ya mikataba miwili kununua jengo la ubalozi lenyewe tu inaunda kosa la jinai,” alisema Hakimu Mugeta. Aliongeza kuwa upande wa mashtaka ulijielekeza kwenye kutambua kama kulikuwa na kibali cha kutumia mikataba miwili au la. “Sidhani kama hili linahusiana katika mazingira ya kesi hii. Hii ni kwa sababu kama utumiaji wa mikataba miwili ni kosa la jinai, hakuna kibali ambacho kingeweza kuhalalisha hilo isipokuwa tu kwa kubadilisha sheria husika,”alisisitiza Hakimu Mugeta. Hakimu Mugeta alirejea ushahidi wa utetezi wa Mkapa kuwa hata kama lengo la muuzaji wa jengo hilo lilikuwa ni kukwepa kodi ya nchi yake, hilo ni tatizo la mwenye jengo na nchi yake na kwamba matakwa ya nchi yalikuwa ni kupata jengo la ubalozi. Hakimu Mugeta alisema kwa mujibu wa kielelezo cha 5 cha upande wa utetezi [exhibit D5], taarifa ya mthamini kutoka Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, thamani ya jengo hilo ilikuwa ni Dola za Marekani 5.5milioni. Alisema hata hivyo, tathmini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa bei ya jengo hilo ilikuwa ni Euro 3,098,741.38 na kwamba ndiyo maana ilituma kiasi hicho ambacho ndicho kilicholipwa kwa mnunuzi. Kuhusu shtaka la wizi, Hakimu Mugeta alisema kuwa hakuna ushahidi unaonyesha kuwa baada ya kiasi hicho cha pesa kulipwa kwa mwenye jengo kupitia akaunti mbili tofauti za benki za mwenye jengo, baadaye Mahalu alikwenda benki kuzichukua pesa hizo kwa matumizi yake binafsi. Alisisitiza kuwa mshtakiwa wa kwanza alipewa mamlaka ya kununua jengo hilo kwa bei iliyoonyeshwa katika kielelezo hicho cha 7 cha upande wa mashtaka yaani Euro 3,098,741.38. Hakimu Mugeta alisema kwa maoni yake ni kwamba ikiwa mshtakiwa baada ya Serikali kukubali bei hiyo ya ununuzi wa jengo hilo, kutoa pesa, na kumpa mshtakiwa wa kwanza nguvu ya kisheria, utaratibu wa malipo ulipaswa kufuata taratibu za Italia. Alisema hayo ni masharti ambayo muuzaji alimpa mshtakiwa wa kwanza na kwamba shahidi wa pili upande wa utetezi, Mkapa alisema kuwa mahitaji ya nchi yalikuwa ni kupata jengo. Hakimu Mugeta alisisitiza kwamba kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka na hata wa utetezi, taratibu zote za ununuzi wa jengo hilo zilifuatwa na kwamba ndiyo maana wataalamu walitumwa kwenda kufanya uthamini. Kutokana na makosa hayo kutokuthibitishwa na upande wa mashtaka, Hakimu Mugeta pia alitupilia mbali kosa la kuisababishia hasara Serikali akisema kuwa pia upande wa mashtaka umeshindwa kulithibitisha. Utetezi wa Mkapa Wakati wa utetezi wao, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake alipanda kizimbani na kumtetea Mahalu na mwenzake, akidai kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulifuata sheria. Mkapa katika ushahidi wake wa utetezi licha ya kudai kuwa mchakato huo ulifuata taratibu na kwamba ni yeye aliyebariki, pia alimmwagia Mahalu sifa nyingi akidai kuwa ni kiongozi mwadilifu na mwaminifu katika historia yake ya utumishi wa umma. Akiongozwa na mmoja wa mawakili wanaomtetea Mahalu na mwenzake, Wakili Alex Mgongolwa, Mkapa alieleza mchakato wote wa ununuzi wa jengo hilo na malipo yake kwa kuwa lilinunuliwa kwa maagizo Serikali yake. Wakati upande wa mashtaka ukidai kuwapo kwa uhujumu uchumi kutokana na kuwapo kwa mikataba miwili wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Mkapa alidai kuwa aliifahamu mikataba hiyo yote na malipo kufanyika kupitia akaunti mbili tofauti. Alienda mbali zaidi na kueleza kushangazwa kusikia kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo, Martin Lumbanga katika ushahidi wake alidai kuwa hakujua mchakato wa ununuzi wa jengo hilo, akieleza kuwa haujui ni kwa nini Lumbanga alisema hivyo. Mbali na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyekuwa waziri wake, Mkapa alisema wizara nyingine zilizohusika ni Wizara ya Ujenzi na Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Alidai kuwa wizara zote hizo zilituma wataalamu wake kwenda kufanya tathmini ya thamani ya jengo hilo kabla ya ununuzi wake. Alisisitiza kuwa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Kikwete bungeni juu ya ununuzi wa jengo hilo ni sahihi. Pamoja na mambo mengine taarifa hiyo inaeleza kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa Sh2.9 bilioni na kwamba hati za umiliki wake zilishawasilishwa wizarani na kupelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali [CAG]. “Maneno hayo ni sahihi. Hayo ndiyo ninayoyajua mimi,” alidai Mkapa na kuongeza kwamba hajawahi kupata malalamiko kutoka Italia kuhusu ukiukwaji wa sheria wakati wa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo wala kwa mmiliki akidai kuwa alilipwa pungufu ya makubaliano. Akijibu swali la Wakili Mgongolwa kama alishapata malalamiko yoyote kutoka kwa CAG kuhusu ununuzi wa jengo hilo, alijibu kuwa hajawahi kupokea malalamiko hayo. Akijibu swali la Wakili wa Serikali, Ponsiano Lukosi kama aliwahi kuuliza ni kwa nini mwenye jengo alitaka alipwe kupitia mikataba miwili Mkapa alijibu kuwa hakuuliza kwa kuwa alichokuwa anahitaji ni kupata jengo. Kuhusu kama lengo la mwenye jengo kutaka kulipwa kwa mikataba miwili lilikuwa ni kukwepa kodi ya Serikali ya nchi yake, Mkapa alijibu: “Hilo ni tatizo lake na nchi yake, mimi nilikuwa nataka nyumba na nimepata nyumba, nasema Alhamdulilah”. Pia Mkapa alisema kuwa anamshangaa sana wakili wa Serikali kudai kuwa pesa hizo kulipwa kwa awamu mbili Mahalu alikuwa na lengo za kuzichukua na kuzitumia kwa masilahi yake. “Mimi nitashangaa sana kusikia hivyo na hasa nitakushangaa wewe maana Profesa [Mahalu] mimi namwamini.”, alisisitiza Mkapa. Maoni nje ya mahakama Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mawakili waliokuwa wakimtetea Balozi Mahalu na mwenzake, Martin waliizungumzia hukumu hiyo kwa nyakati tofauti. Wakili Mabere Marando, baada ya Hakimu Mugeta kuwaachia huru wateja wake saa 7:27 mchana alisema kuwa ana furaha kubwa kwa kuwa Mahakama imetenda haki. “Hukumu hii iliyotolewa leo kweli ni ya kihistoria kwa sababu ni hukumu ya haki, hakimu amejitahidi kueleza hoja na zote ni za muhimu na kwamba hapakuwepo na sheria ya kumshtaki Mahalu,”alisema Marando huku akiwa ni mwenye tabasamu. Wakili Alex Mgongolwa ambaye naye pia alikuwa akiwatetea kina Mahalu, alisema kuwa ana furaha kwa kuwa haki imetendeka. “Kwa kweli haki imeonekana kutendeka na imetendeka; Mahakama imetenda haki,”alisema Mgongolwa huku akicheka. Naye Martin alisema: “Namshukuru Mungu kwa kushinda kesi hii.” Wakati hayo yote yakiendelea mahakamani hapo, ndugu wa Mahalu na Martin walikuwa na furaha huku wakituma ujumbe mfupi kweye simu zao za mkononi wakiwajulisha wenzao juu ya tukio hilo. Katika utetezi wao, upande wa Jamhuri ilileta jumla ya mashahidi saba ambao ni aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Martin Lumbanga, Stewart Migwano, Marco Papi, Kapteni Abubakari Ibrahim, Mkongoti, Kyando kutoka Takukuru na nyaraka mbalimbali. Utetezi wa Mahalu Awali akitoa utetezi wake katika mahakama hiyo, Mahalu alidai kuwa alipofika katika Ubalozi huo wa nchini Italia alikuta ofisi zikiwa na hali mbaya hali iliyosababisha kutoa fedha zake mfukoni na kununua thamani zenye hadhi ya ofisi ya ubalozi. Akiongozwa kutoa utetezi wake na wakili wake Marando na Mgongolwa alidai kutokana na kuikuta ofisi hiyo ikiwa na hali hiyo mbaya alilazimika kutoa fedha zake mfukoni kwa ajili ya kununulia samani za ofisini. Mahalu alidai kuwa Aprili 1, mwaka 2000 ndiyo siku aliyofika rasmi mjini Rome nchini Italia ikiwa ni siku chache baada ya Mkapa kumteua kuwa Balozi ambapo alieleza majukumu yake yalikuwa ni kulinda na kuyatetea masilahi ya Tanzania na wakati akiwa Balozi wa Italia pia wakati huo huo alikuwa ni balozi wa nchi tisa ambazo ni Greece, Turkey, Serbia, Slovenia,Croatia, Macedonia, Montenegro. Alieleza jukumu lake jingine ni kupokea maelekezo kutoka hapa nchini kuhusu kukuza uhusiano baina ya nchini na nchi na kwamba yeye ndiye aliyekuwa mkuu wa masuala yote ya utawala wa ofisi ya ubalozi na kwamba masuala yote ya utawala yalikuwa yakiletwa kwake na maofisa wa ubalozi na Serikali kwa ujumla. “Nilipofika Italia nilikuta hali ni mbaya inasikitisha kwani ubalozi wa wetu nchini Italia ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1994 na nilipoteuliwa mimi kwenda huko ndiyo nikawa nimeenda kuufungua ubalozi huo uanze kufanya kazi. Na wakati nafika hapo kila kitu cha ubalozi kilikuwa kimeondolewa na kurudishwa nchini kikabaki kiofisi kidogo tu kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kilimo na mwaka 1997 ndiyo Serikali ilimpeleka msimamizi wa ofisi hiyo.” Alidai kuwa baada ya kukuta hali hiyo alichukua hatua ya kumweleza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa wakati huo, Balozi Kibeloh na kwamba aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo kwa kipindi hicho alikuwa Jakaya Kikwete ambaye kwa sasa ndiye Rais wa nchi ambaye naye alifika katika ofisi za ubalozi huo na kushuhudia hali hiyo mbaya. Alidia Kikwete aliunga mkono hoja yake kwamba ofisi hiyo ni mbovu na akashauri ipatikane ofisi yenye hadhi ya ubalozi. Aliendelea kueleza mbali na Kikwete, pia aliyekuwa Makamu wa Rais , Dk Ali Mohamed Shein naye alitembelea ofisi hizo za ubalozi na kushuhudia ubovu ule na akamuahidi mshtakiwa huyo kuwa akirudi nchini atafikisha tatizo hilo ili taratibu zifanywe za kupatikana jengo kubwa la ubalozi. Profesa Mahalu alieleza kuwa baada ya kumweleza matatizo hayo ya ubalozi Katibu Mkuu, Balozi Kibeloh, alikubaliana naye akasema ni muhimu kwa Serikali kutafuta jengo jipya na kwamba Mei 2001, alipewa taarifa na balozi huyo kuwa Rais Mkapa atakwenda Brussels kwa ziara ya kikazi na kwamba yeye mshtakiwa akamwomba tena katibu mkuu huyo amruhusu akamweleze Mkapa matatizo hayo pindi atakapofika Brussels na katibu mkuu huyo alimruhusu. “Niliporudi mjini Rome Italia, nilimjulisha kwa barua Katibu Mkuu Balozi Kibeloh mazungumzo yangu na Rais Mkapa na balozi huyo naye akanijibu kuwa atazidi kulifuatilia jambo hilo na kuliweka kwenye bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na kwa sababu hiyo ilikuwa ni sera ya wizara yake ya kutaka ofisi za ubalozi wetu nje ya nchi zinunue majengo yao hivyo hoja hiyo itapelekwa bungeni na haitapingwa. ”alidai Profesa Mahalu. Mshtakiwa huyo aliendelea kueleza kuwa wakati akisubiri ahadi hiyo ya Katibu Mkuu huyo, mwanzoni mwa Juni 2001, Katibu Mkuu huyo alimpigia simu akimpongeza kwamba maombi ya wizara yao katika bajeti ya kutaka kila ofisi ya ubalozi inunue jengo lake itapitishwa na Bunge na kuongeza kuwa Katibu Mkuu alimtaka mshtakiwa huyo na maofisa wengine wa ubalozi kuanza kutafuta majengo. Alidai kuwa baada ya kupokea habari hiyo njema kutoka kwa Katibu Mkuu, yeye mshtakiwa alimwandikia barua ya kumshukuru Mei 4 mwaka 2009 ambayo nakala yake aliomba mahakama iipokee kama kielelezo na Hakimu Mugeta aliipokea kama kielelezo cha kwanza. Utetezi wa Grace Mei 8, mwaka huu, Martin ambaye alikuwa Ofisa wa Utawala aliieleza mahakama hiyo ya Kisutu kuwa Balozi Mahalu hakuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni, bali alileta faida kwa taifa kwa kuwa na jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani. Akiongozwa na Wakili Marando kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili, Martin alidai kuwa kwa ufahamu wake Balozi Mahalu hakuisababishia Serikali hasara kwa kuwa ununuzi ulileta faida na nchi kupata jengo zuri na fedha hazikupotea na anastahili shukrani. Aliendelea kuiomba Mahakama itupilie mbali tuhuma hizo na kwamba madai ya kuwa Balozi Mahalu alitumia risiti ya ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia kuidanganya Serikali kuwa mwenye nyumba amelipwa fedha siyo ya kweli.
Popular Posts
-
What to do in Zanzibar when you’re a tourist? I had booked myself a 4-day trip to the island, and, taking the advice of friends and a quic...
-
Ujerumani imerejesha mafuvu ya Wanambia ishirini waliofariki dunia baada ya fujo dhidi ya utawala wa ukoloni wa Kijerumani zaidi ya miaka 1...
-
Uingereza imesitisha kwa muda msaada iliyokuwa iipe Rwanda kwa sababu ya wasiwasi kuhusu kuhusika kwa nchi hiyo katika mzozo uliopo Jam...
-
Huduma ya Maji na Nishati (EWURA), Mhandisi Godwin Samwel, akizungumza na wanahabari jana jijini, Dar es Salaam kuhusu kupanda kwa bei za m...
-
MSANII wa kughani, Mrisho Mpoto, amesema kuwa anaamini mavazi yanatosha kuutambulisha muziki wake na hivyo hatarajii kubadili aina ya mav...
-
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba amesema moja ya mambo yaliyohojiwa na wananchi wengi katika mchaka...
-
Chuo kikuu cha Zanzibar (Zanzibar University) Kikitoa utambulisho na ukaribisho kwa wanafunzi wa Shahada ya Kwanza pamoja na wanafunzi wa S...
-
Timu ya mpira wa miguu ya makao makuu ya bandari(picha kwa hisani ya bandari) Katibu Mkuu wa Dowuta Taifa, Bw. Jonathan Msoma a...
-
Maandamano kupinga uroho wa makampuni yamefanywa sehemu mbali mbali za dunia, yakitiwa moyo na maandamano ya wiki mbili sasa yanayofanywa N...
-
HERIETH MAKWETTA MSANII wa muziki wa kizazi kipya kutoka Tanzania, Rehema Chalamila maarufu kama Ray C, yupo katika kituo maalumu cha msa...
Habari Leo Tanzania, Media, (East Africa)
0 comments:
Post a Comment