Nundu akaribisha ushindani wawekezaji hoteli za kitalii

Sunday, September 4, 2011


WAZIRI wa Uchukuzi, Omary Nundu, amesema kufunguliwa kwa Hoteli ya Kitalii ya Nyumbani, utaongezeka ushindani kwa sekta hiyo, huku ikiwa ni kichocheo cha ufufuaji na ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Tanga.

Akifungua Hoteli ya Nyumbani juzi, Waziri Nundu alisema ameanza kufarijika kwa kujitokeza wawekezaji wazalendo kufufua uchumi wa mkoa huo na kwamba, watalii watakaotaka kuja hawana sababu ya kujiuliza sehemu watakayofikia.

“Vitega uchumi hivi ndivyo vinavyofanya Tanga kuwa jiji. Nimeshuhudia vitu mbalimbali ndani ya hoteli hii, nimetembea duniani na ninaposema nimetembea ni kweli nimetembea, hakuna tofauti na nilivyoona hapa,” alisema Nundu na kuongeza: “Nafarijika kuwa wageni hao wakitaka kuja kuna sehemu ya kufikia kama walivyozoea.”

Pia, aliwataka wamiliki wa hoteli hiyo kuongeza idadi ya vyumba na kwamba, kauli yao kuwa hawahitaji ushindani siyo sahihi.

“Naona wametumia lugha ya kidiplomasia kuwa hawataki ushindani. Hapana! Tunataka ushindani wa biashara kwenye huduma, siyo kutunishiana misuli,” alisema N undu.

Kuhusu ahadi ya wawekezaji kuwa watanunua bidhaa kutoka mkoani hapa, Waziri aliwataka wananchi wa hapa wa kilimo na mazao ya viwandani kuongeza ubora wa bidhaa, huku akiwasihi wananchi wa hapa kuiona hoteli hiyo kama mali yao, kwa sababu inazidi kuongeza ajira.

Pia, alisema ombi la wawekezaji hao kupatiwa maeneo kwenye viwanja vya ndege nchini kujenga hoteli, litafanyiwa kazi hasa kipindi hiki wanapotarajia kuongeza abiria wanaoingia nchini kutoka milioni 1.5 kwa mwaka hadi milioni sita, baada ya kukamilika ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Awali, akimkaribisha Waziri Nundu, Mkurugenzi wa Nyumbani Hoteli, John Kessy, alisema mradi huo umetumia zaidi ya Sh3.5 bilioni na kwamba, ni mtandao wa hoteli ambazo tayari zimejengwa Mwanza, Kilimanjaro na wanaendelea na mikoa mingine.

Kessy alisema wanaomba Serikali kupewa fursa na eneo uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, Kilimanjaro na viwanja vingine kujenga hoteli za nyota tano.

Akimshukuru Waziri Nundu, mmoja wa wakurugenzi, Aloyce Kimaro, alisema hotuba yake imewafariji na wamekwenda kufanya biashara, siyo malumbano na kuomba kuona kitega uchumi hicho kama rasilimali ya mkoa.

0 comments:

Post a Comment