RAIS wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuandaa chakula cha hisani Oktoba 18, mwaka huu kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), kwa wahitimu wote waliosoma katika Chuo hicho.Ujenzi huo utalenga kuongeza vyumba vya wanafunzi wa chuo hicho ,ambacho kinakabiliwa na uhaba wa vyumba vya kupumzikia, maktaba na sehemu za viburudisho.
Taarifa hiyo ilitolewa na Rais wa waliohitimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juzi katika chuo hicho.
Warioba alisema kuwa , wakati ambapo Chuo kinaadhimisha miaka 50 ya uhuru tangu kuanzishwa kwake idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na wakati walipokuwa wakisoma wao chuoni hapo.
Amesema chuo hicho kilipoanza kilikuwa na jumla ya wanafunzi 14 wakati kwa sasa idadi ya wanaoingia chuoni hapo inakadiriwa kufikia hadi wanafunzi 20,000 kwa mwaka.
Alisema kuwa kutokana na wingi wa wanafunzi hao wamefikia hatua ya kukosa sehemu ya kupumzikia, kujisomea na kufanya mambo mengine yanayohusu taaluma kutokana na majengo ya chuo hicho kuwa machache ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo.
“Tumeona huu ni wakati mzuri wa kuchangisha fedha za ujenzi wa vituo vya wanafunzi hasa kwa wahitimu wote waliosoma katika chuo hiki kwa kushiriki chakula cha hisani na Rais ili kuona kama tutaweza kunusuru hali hii inayowakabili wanafunzi wanaosoma katika chuo hiki ,”alisema Warioba.
Jaji Warioba, alisema kuwa wahitimu wote wanaombwa kujitokeza kwa wingi siku hiyo ya Jumanne kumuunga mkono Rais Kikwete katika hafla hiyo itakayofanyika katika ukumbi wa Mlimani City kuanzia saa 12:30 jioni.
Alisema kuwa hadi sasa baadhi ya waliohitimu chuoni hapo wamekwishachangia zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya mpango huo na kuwaomba wengine kuendeleza jitihada hizo.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es salaam , Profesa Rwekaza Mukandala, alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho unatarajia kuanza Aprili 2012 na utakamilika katika kipindi cha miezi 26.Alisema kuwa kwa sasa wanafunzi wa chuo hicho wamekuwa wakitaabika kupata sehemu za kujisomea na kufanyia shughuli nyinginezo sambamba na tatizo la maabara .
“Tunawategemea sana waliohitimu katika chuo hiki kutuwezesha katika harakati za ujenzi wa huu ili watoto wetu wasisumbuke maana zamani idadi ya wanafunzi haikuwa kubwa kama ilivyo sasa, tunawaomba wajitokeze kwa wingi,” alisema Profesa Mukandala.
Alisema kuwa kwa yeyote atakayetaka kuchangia au kutoa ahadi anaweza kutumia namba za simu zifuatazo:0753-410514/0658410514/0784314688 au akaunti namba 01J1088967004 UDSM Students Centre.
0 comments:
Post a Comment