Waandishi Wetu, Dar na Moshi
IKULU imesema Rais Jakaya Kikwete hahusiki na utoaji wa msamaha wa kupunguza adhabu ya kifo iliyotolewa na Mahakama kwa askari polisi wa zamani waliopatikana na hatia ya kumpiga risasi na kumwua kwa makusudi aliyepata kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe.Kwa taarifa hiyo ya Ikulu, inamaanisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Benjamin Mkapa ndiyo iliyohusika na msamaha huo.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa juzi haikumtaja moja kwa moja Mkapa lakini iliweka wazi kuwa uamuzi huo ulifanywa na serikali yake ambayo ilikuwa madarakani wakati polisi hao walipohukumiwa na Mahakama Kuu mwaka 1998. Mkapa alikuwa madarakani kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano, kuanzia 1995 na 2000 na kisha 2000-2005.
“Masuala yote yanayohusu polisi hao waliohukumiwa kifo kwa mauaji ya Luteni Jenerali Kombe yalifanyiwa maamuzi kabla ya Rais Kikwete kuingia madarakani Desemba 21, 2005,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.
Lengo la taarifa hiyo ya Ikulu ilikuwa ni kukanusha taarifa zilizoandikwa na gazeti hili kuhusu polisi hao wawili kuachiwa huru hivi karibuni.Katika taarifa hiyo, Ikulu inapinga habari zilizotolewa na gazeti hili Jumatano na Alhamisi wiki hii zikidai kuwa Rais Kikwete ndiye aliyetoa msamaha huo baada ya kupunguza adhabu yao hadi miaka miwili.
Wakiwa askari wapelelezi, Koplo Juma Muswa na Konstebo Mataba Matiku walihukumiwa kunyongwa hadi kufa mwaka 1998 baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi Luteni Jenerali Kombe Juni 30, 1996.
Kombe aliuawa kwa kupigwa risasi nne kifuani Juni 30, 1996 baada ya polisi waliokuwa wakisaka gari aina ya Nissan Patrol, mali ya W. Ladwa kumfananisha na mtuhumiwa sugu wa wizi wa magari.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Matiku alidai kuwa walitoka gerezani Mei, mwaka huu walikokuwa wakisubiri kutekelezwa kwa adhabu yao ya kunyongwa, kabla ya Rais kuwaonea huruma na kuwapunguzia adhabu.
“Unajua baada ya Jaji kutuhukumu kunyongwa tulikata rufaa, Mahakama ya Rufani ambayo iliona ile hukumu ilikuwa ni sahihi ikasema tuendelee nayo hadi tulipoomba huruma ya mheshimiwa Rais,” alisema Matiku.
Matiku alisema jopo lililomshauri Rais lilipendekeza wapunguziwe adhabu kutoka kunyongwa hadi kifungo cha miaka miwili na kwa kuwa walikuwa mahabusu tangu 1998, kifungo hicho kilitosha.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wanasheria, wasomi na watu wa kawaida wametoa maoni tofauti wakishangazwa na uamuzi huo wa Ikulu wakihoji iweje Serikali iliyomtangulia Rais Kikwete itoe uamuzi wake na utekelezaji wake ufanyike miaka saba tangu utawala mwingine uingie madarakani.
“Kauli ya Ikulu si sahihi hata kidogo, nadhani wasaidizi hawakufanya vizuri kwa sababu Urais ni taasisi. Hata asipokuwepo Kikwete leo bado atakayefuata atazungumzia uamuzi uliofanywa naye akiwa Rais na siyo mtu binafsi,” alisema wakili mmoja ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Alisema uamuzi wa kuwapunguzia adhabu polisi hao ulifanywa kwa kuzingatia madaraka ya Rais aliyopewa Kikatiba chini ya Ibara ya 45 ya Katiba ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2008.
“Kwa nini Ikulu inapiga danadana wakati ni suala la kikatiba? Ikulu ilitakiwa kusema ni Rais fulani alifanya uamuzi huo kwa sababu umma unataka kujua lakini kutoa statement (taarifa) ambayo inaacha maswali mengi zaidi nalo ni jambo la hatari sana” alisema wakili huyo.
Mkazi mmoja wa Mailisita alikouawa Kombe, alisema jana kuwa anashangazwa na taarifa hiyo ya Ikulu kutoeleza ilivyokuwa akisema kama uamuzi haukufanywa na Rais Kikwete ilikuwaje utekelezwe katika kipindi chake wakati Mkapa alishaondoka madarakani 2005?
Ibara hiyo ya Katiba kifungu kidogo cha 1(a) na (b) kinampa Rais madaraka ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama na hata kubadilisha adhabu yeyote kwa kosa lolote ili iwe adhabu tahafifu.
Mauaji ya Luteni Jenerali Kombe yaliyotokea mkoani Kilimanjaro yaliibua minong’ono mingi kwamba huenda yalitokana na hatua ya marehemu kuonekana kuunga mkono upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 1995.
Kutokana na minong’ono hiyo, Serikali iliunda tume chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Damian Lubuva na Jaji Mussa Kipenka wakati huo akiwa mwanasheria mwandamizi wa Serikali, kuchunguza tukio hilo.Hata hivyo, taarifa ya tume hiyo imeendelea kuwa siri hadi leo.
0 comments:
Post a Comment