KUTOKANA na kile kichoonekana ni kutaka kukabiliana na uhaba wa sukari na kupanda kwa bei yake, Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatarajia kukutana na mawaziri wawili kujadili kiini cha tatizo hilo na kutafuta ufumbuzi wake.
Tayari maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na baadhi ya Kanda ya Ziwa, imekumbwa na uhaba mkubwa wa sukari na kusababisha bei ya bidhaa hiyo, kupanda.
Habari kuhusu Waziri Mkuu kutaka kukutana na mawaziri hao wawili, ili kuzungumzia tatizo hilo, zilitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Dk Cyril Chami.
Waziri huyo alikuwa akijibu maswali kuhusu kupanda kwa bei ya sukari hapa nchini.Mawaziri wanaotarajia kukutana na Pinda wakati wowote kuanzia sasa ni Dk Chami na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,Profesa Jumanne Maghembe.
Dk Chami alisema kukiukwa kwa maagizo ya serikali yalitolewa hivi karibuni kuhusu bei ya sukari, kunatokana na vitendo vya baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakisafirisha bidhaa hiyo kwenda nchi jirani inakouzwa kwa bei kubwa.
“Tunakutana kujadili suala hili wakati wowote kuanzia sasa, lakini uchunguzi uliofanywa na serikali umebaini kuwa sukari imeadimika katika jirani za Kenya, Uganda na Rwanda ambako bei ya sukari imepanda maradufu,”alisema Dk Chami.
Dk Chami alizitaja nchi zingine zinazokabiliwa na uhaba wa sukari kuwa ni Kenya na Somalia.Alisema kisingi, serikali inatarajia kuchukua hatua za haraka kuangalia upya bei ya bidhaa hiyo na kupiga marufuku sukari kusafirishwa nje ya nchi , kama itaona inafaa.
“Kwa sasa tuko kwenye kipindi cha biashara huria,lakini zaidi Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashiarika, ambayo imeondoa ushuru wa forodha kwenye bidhaa zinatoka nje, hii imetoa mwanya kwa wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kusafirisha sukari kwenda nje ya nchi,”alisisitiza Dk Chami.
Alisema kwa singi huo, kikao cha Waziri Mkuu, kinatarajia kuja na mkakati utakaowezesha kukabilina na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakipandisha bei ya sukari na hata kusafirisha kwenda nje ya nchi.
“Sisi kama serikali tutachukua hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku sukari kuuzwa nje kama ilivyokuwa kwenye mahindi ,lengo letu ni kuhakikisha kuwa sukari inakuwapo nchini na kwa bei inayokubalika,”alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Dk Chami alielezea kushangazwa kwake na ukimya wa Bodi ya Sukari Tanzania ambayo alisema ndiyo yenye jukumu la kusimamia uzalishaji na uuzaji wa sukari.Alisema sheria inaipa bodi hiyo mamlaka ya kusimamia uzalishaji wa sukari na usambazaji wake na kusisitiza kuwa ndio yenye jukumu la kuhakikisha bei inakuwa ya namna gani.
Hivi karibuni Bodi ya Sukari Tanzania, ilitaja sababu za kupanda kwa bei ya sukari hapa nchini kuwa ni pamoja na baadhi ya wafanyabiashara, kujihusha na vitendo vya magendo ya kusafirisha sukari kwenda nje ya nchi.
Sababu nyingine ni uzalishaji mdogo ikilinganishwa na mahitaji ya tani 500,000 kwa mwaka wakati uzalishaji ukiwa ni tani 300,000 kwa mwaka.
0 comments:
Post a Comment