Mrisho Mpoto:Mavazi ndo utambulisho wangu

Saturday, September 3, 2011


MSANII wa kughani, Mrisho Mpoto, amesema kuwa anaamini mavazi yanatosha kuutambulisha muziki wake na hivyo hatarajii kubadili aina ya mavazi yake siku za usoni.

Mpoto ambaye amejizolea umaarufu kutokana na mashairi yake yanayowagusa wengi, amesema uvaaji wake unazingatia mila na desturi za Mtanzania na hivyo haoni sababu ya kubadili staili yake ya uvaaji.

"Unajua wengi sana huwa wananiuliza kuhusu uvaaji wangu, ni kweli hata ukiniona mtaani mara nyingi ninavaa hivi, si kwamba sanaa pekee imenifanya nivae hivi, la! bali ninahisi napaswa kuvaa hivi, hivyo sina mpango wa kubadili staili yangu" alisema.

Mghani huyo wa mashairi aliongeza kuwa ni vema wananchi na wasanii kwa ujumla wakajali na kuthamini vya kwao kuliko kushabikia vya wengine na kudharau kule walikotoka.

"Tukumbuke asili yetu jamani...! si tunavaa vichupi na hata milegezo ambayo ni ya Wamarekani au mataifa mengine, mbona ukivaa hivi unapendeza na kuwavutia wengi? tujali na kuthamini vya kwetu, na katu tusidharau vya kwetu" alisisitiza.

Hata hivyo Mpoto alisema kuwa hajawahi kufanya kazi nyingine tofauti na sanaa na kwamba hatarajii wala hategemei kufanya kazi nyingine hapo baadaye.

"Unajua sijawahi fanya kazi tofauti na sanaa, tangu ningali mdogo nimekuwa kwenye sanaa na mpaka sasa nashughulika na sanaa kiasi kwamba imenizoea nami nimeizoea ndio maana ninapopata hisia inaniwia rahisi kuimba wimbo wenye mafunzo" alisema.

Mpoto anayetamba na kibao chake cha Bure hivi sasa, amesema kuwa kibao hicho ni historia ya kweli kwani dada yake alifariki kutokana na ugonjwa wa TB hivi karibuni.

0 comments:

Post a Comment