Mapigano makali katika mji wa Galkayou, kati ya Somalia, yameuwa watu kama 30 na mia moja kujeruhiwa.
Mji huo uko baina ya Puntland na Galmudug, na Puntland inasema mapigano hayo yalikuwa baina ya wanajeshi wake na kikundi chenye uhusiano na al-Shabaab.
Wakati huo huo shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na wakimbizi, UNHCR, limeonya kuwa hali katika nchi ya Somalia iliyopigwa na ukame, inazidi kuwa mbaya na karibu maeneo yote ya kusini mwa nchi yanaweza kukabili njaa.
UNHCR inasema utapia mlo na idadi ya watu wanaokufa inaongezeka, na magonjwa yanazidi kutapakaa.
Shirika hilo linasema lina taarifa kuwa wapiganaji wa Kiislamu wa al-Shabaab - ambao wanadhibiti eneo la kusini la Somalia - bado wanazuwia nyendo za watu katika eneo hilo.
Watu zaidi ya milioni 12 wameathiriwa na ukame katika pembe ya Afrika.
Na kwa mara ya kwanza Umoja wa Mataifa unapanga kufanya mkutano maalum kuhusu mustakbali wa Somalia ndani ya nchi hiyo.
Mazungumzo ya siku tatu yatayojumuisha wahusika wote, kuhusu suala la Somalia, yataanza kesho mjini Mogadishu.
0 comments:
Post a Comment