WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli, ametangaza kiama kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam ambao wamejenga ama wanaendesha shughuli zao katika hifadhi ya barabara, akieleza kuwa wote watakumbana na dhoruba ya bomoabomoa wakati wowote kuanzia sasa.
Tamko hilo la Dk Magufuli ni kama lile alilolotoa mwezi Januari mwaka huu, kabla ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kusimamisha utekelezaji wake, huku Rais Jakaya Kikwete naye akimtaka apunguze makali ingawa anatumia sheria na badala yake kuingiza suala la ubinadamu.
Lakini safari hii Dk Maghufuli amekuja kwa mtindo ule ule lakini hakuweka wazi
ni lini hasa operesheni itaanza kutekelezwa na wala kama maagizo ya Rais Kikwete na Waziri Pinda, atayazingatia.
Dk Magufuli aliwaambia waandishi wa habari jana Jijini dar es Salaam kuwa mkakati huo anautekeleza kama sehemu ya mafanikio ya sekta hiyo miaka 50 ya uhuru wa Tanzania.
Alisema Wizara yake itashirikiana na Jeshi la Polisi Kanda Maalum yaDar es Saalam, katika utekelezaji wa operesheni hiyo ambayo alisema ni sehyemu ya utekelezaji wa mpango wa kupunguza msongamano jijini humo.
“Tayari tumezungumza na polisi juu ya utekelezaji wa sheria (kuwaondoa watu waliovamia hifadhi ya barabara), ili kuondoa msongamano kwenye jiji la Dar es Salaam tutabomoa majengo yaliyojengwa kwenye hifadhi ya barabara na tutawaondoa wale wote wanaofanya biashara katika maeneo hayo,” alisema Dk Magufuli na kuongeza:
“Sisi tunafanya kazi kwa kufuata sheria kwa hiyo wale wote wavunjifu (wanaovinja) wa sheria watachukuliwa hatua, lengo letu ni kuhakikisha barabara zinajengwa na foleni zinamalizika Dar es Salaam.”
Msimamo wa kuendelea na bomoabomoa alioutoa Dk Magufuli jana, aliwahi kuutoa tena mbele ya Rais KIkwete, wakati wa uzinduzi wa upanuzi wa barabara Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 12.9.
“Katu sitaacha kusimamia sheria namba 18 ya mwaka 2007 ambayo ilisainiwa na Rais mwenyewe inayokataza watu kuingilia eneo la hifadhi ya barabara kwa kujenga makazi au kufanya biashara,” alizungumza Dk Magufuli Mbele ya Rais Kikwete.
Wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya wizara yake bungeni Dodoma, Dk Magufuli alisema jiji la Dar es Salaam haliwezi kubadilika ikiwa kutakuwa na ulegevu wa kusimamia sheria huku akisema watu wenye fedha wamekuwa wakimkwaza kutekeleza wajibu wake.
Kikwete na Pinda
Katika mpango kama huo alioutangaza mapema mwaka huu siku chache baada ya kurejeshwa katika Wizara ya Ujenzi, Dk Magufuli alikumbana na kizingiti pale Waziri Mkuu, Pinda na Rais Kikwete kwa nyakati tofauti, walipomtaka kuachana na mpango huo wa bomoabomoa ambao tayari ulishaanza kutekelezwa kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Pinda akiwa ziarani mkaoni Kagera, mbele ya Magufuli alitangaza kusitishwa kwa bomoabomoa hiyo, na kutaka wakuu wa mikoa wafanye tathmini ya kina juu ya madhara ya utekelezaji wa mpango huo ili kuwa na uhakika wa idadi ya nyumba zitakazoguswa na jinsi serikali inavyoweza kusadia kulipa fidia.
Pinda alisema kasi aliyoanza nayo Magufuli katika wizara yake mpya imeitisha serikali na kuwa ameagiza kusimamisha zoezi hilo mpaka litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri.
“Rais aliona kwenye barabara panalegalega na kumrudisha Magufuli kwenye wizara hiyo, huyu serikalini tunamwita ‘buldoza’ hata hivyo ameanza kwa speed kubwa na tumwemwagiza asimamishe zoezi hilo mpaka litakapojadiliwa na Baraza la Mawaziri,”alisema Pinda.
Naye Rais Kikwete alipinga zoezi hilo alipotembelea Wizara ya Ujenzi, ambapo aliwataka watendaji wa wizara hiyo kuacha kuwa wababe na kuwataka waendeshe operesheni ya bomoabomoa kwa sura ya utu.
Kikwete alimuagiza Dk Magufuli kulegeza sheria na kuangalia pia ubinadamu ikiwa ni pamoja na kuwalipa wote wanaostahili fidia na kwamba wasiangalie tu mazingira ambayo yataepusha mzigo wa gharama kwa Serikali.
''Hili naliongea kwa umakini kwani nataka nieleweke vizuri. Bomoabomoa ipo. Usilegee katika kutekeleza sheria, lakini uangalie ubinadamu katika bomoa hiyo pamoja na historia ya eneo husika,”alisema Kikwete.
Mikakati mingine
Dk Magufuli alitaja mikakati mingine ya kupunguza msongamano wa magari barabarani kuwa ni pamoja na kujenga barabara ya juu kwenye makutano ya barabara Mandela na Nyerere ambayo usanifu wake ulianza Juni mwaka huu.
Mkakati mwingine ni kupanua mtandao wa barabara, kujenga na kukarabati barabara mbalimbali za Jiji zikiwemo zile za Ubungo Bus Terminal kupitia Mabibo na Kogogo zenye urefu wa Km 6.4.
Barabara nyingine ni Kigogo kupitia Bonde la Msimbazi mpaka Twiga/Msimbazi yenye Km 2.7 na kwamba kazi ya ujenzi wa barabara hizo inaendelea na inategemewa kukamilika mwakani.
Alisema katika kusimamia sheria, wakandarasi 2008 wazalendo ambao walijenga barabara chini ya kiwango, wamefutiwa leseni huku akisema wengine ambao hawapo makini watafuata njia hiyo.
“Tena sio Makandarasi tu, wahandisi washauri nao sasa watakiona, sisi kazi yetu ni kusimamia sheria tu,” alisema Dk Magufuli
Akielezea mafanikio ya sekta hiyo, alisema tangu mwaka 1961, mtandao wa barabara umekuwa kutoka Km 33,600 zilizokuwepo mwaka 1961 mpaka Km 86,472 mwaka 2011.
Kwa upande wa mtandao wa barabara za lami, alisema umeongezeka kutoka Kilometa 1,360 mwaka 1961 mpaka Km 6,500 mwaka huu na kuwa Km 11,154 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
0 comments:
Post a Comment