KAMPUNI ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti imetoa msaada wa kilo 200 za mchele na kilo 100 za nyama kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu wa ambao wamekusanywa na Mfuko wa Ali Hassani Mwinyi katika kituo kilichoko Tabata, Jijini Dar es Salaam ili wavitumie wakati wa Sikukuu ya Eid- El Fitr.
Msaada huo pia ni pamoja na lita 40 za mafuta ya kupikia na kwamba vyote vina thamani ya Sh940,000.
Akizungumza machache baada ya kupokea msaada huo, Katibu wa kamati maalumu ya maandalizi ya sherehe za Eid El Fitr, kwa waoto hao, Omary Njani alisema watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wanakabiliwa na matatizo mengi yakiwemo ya kukosa furaha wakati wa sikukuuu kutokana na kukosa vyakula na vinywaji.
Alisema watoto hao mpia wanakosa masuala ya elimu, mavazi mazuri na hata upendo kutokana na ukweli kwamba ni yatima na wanaishi bila uangalizi wa mtu yeyote mwenye upendo wa kweli.
Alipongeza kampuni ya MCL kwa msaada huo na kuzitaka taasisi,kampuni na jamii kwa ujumla kuiga mfano huo. “Tunapenda kuishukaru kampuni ya Mwananchi Communications Limited kwa kutupatia msaada wa vyakula, lakini pia tunaiomba jamii nyingine zijitokeze kuwasaidia watoto waishio katika mazingira magumu ili nao wapate nafasi ya kujipitia mahitaji muhimu ya kibinadamu,” alisema Njani.
Kwa upande wake, Mhariri Mkuu Mtendaji wa MCL, Theophil Makunga alisema kampuni yake imetoa msaada huo walau kidogo ikiwa ni kuthamini jitihada zinazofanywa na taasisi binafsi kuwasaidia watoto ili waishi maisha ya kawaida.
Makunga alisema watoto ni taifa la kesho ambalo litakuja kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na kwamba watoto wanaoshi katika mazingira magumu hawana budi kusaidiwa wapate faraja na furaha kama wengine.
“Kampuni inatambua mchango wa watoto katika jamii kwani ni viongozi wa baadaye na pia ni wanunuzi na wasomaji, wa magazeti ya MwananchiCommunications Limited wa baadaye”, alisema Makunga. Makunga aliwatakia kila la hewri kwa sikukuuu ya Idd El Fitr watoto hao na kuwataka wasife moyo bali watumie bidii na maarifa wanapopata mwanya wa kupata elimu. Kituo hicho kina watoto 50 wanaoishi katika mazingira magumu.
0 comments:
Post a Comment