Wazalishaji na wasambazaji wa nishati ya gesi kutoka Kisiwa cha Songosongo, SONGAS wameishauri serikali kuwashirikisha wadau wengine ikiwemo sekta binafsi katika uzalishaji wa nishati ya umeme ili kupunguza matatizo ya upungufu wa umeme hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kuzalisha nishati ya gesi ya SONGAS Christopher Ford amewaeleza waandishi wa habari waliotembelea vinu vya kuzalisha na kusambaza umeme kuwa umefika wakati wa sekta binafsi kupewa fursa ya kushiriki katika uzalishaji wa nishati hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Ford amesema SONGAS inazalisha kiwango kinachozidi uwezo wake wa megawati 70 hadi kufikia 180 ili kusaidia kuboresha uzalishaji wa nishati hiyo katika kituo cha Ubungo ili kukabiliana na mgao unaoendelea nchini.
Kwa upande wake Meneja Mkuu msaidizi wa Kampuni ya Pan African Energy yenye dhamana ya kusambaza nishati ya gesi kutoka kampuni ya SONGAS, Willium Chiume amesema serikali inawajibika kutafuta vyanzo vingine vya kuzalisha umeme na kupunguza utegemezi wa umeme wa maji ambao umeendelea kuathiriwa na upungufu wa maji katika mabwawa mbalimbali
0 comments:
Post a Comment