MAAMUZI YA KAMATI KUU YA CHADEMA KUWAVUA UANACHAMA DKT. KITILA NA MWIGAMBA

Wednesday, January 8, 2014

UTANGULIZI 
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilikaa kikao cha dharura ili kupokea, kujadili na kuamua juu ya utetezi wa mashtaka ya ukiukaji wa Katiba, Kanuni na Mwongozo wa Chama yaliyokuwa yanawakabili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto Zuberi Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Arusha Samson M
wigamba. Kikao hicho cha dharura kilifanyika Dar es Salaam kati ya tarehe 3-4 Januari, 2014. Kabla ya kuanza kwa kikao, Kamati Kuu ilipokea taarifa kwamba Zitto Zuberi Kabwe amefungua mashtaka dhidi ya CHADEMA katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. Aidha, Kamati Kuu ilijulishwa kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio la muda ya kuizuia Kamati Kuu au chombo kingine cha Chama kutokukaa, kujadili na kuamua suala la uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe. Kutokana na amri hiyo ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu haikujadili na kuamua juu ya mashtaka dhidi yake.
MASHTAKA
Watuhumiwa wote watatu walishtakiwa jumla ya mashtaka 11 yanayohusu ukiukaji wa vifungu mbali mbali vya Katiba ya Chama, Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama, Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa Chama na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali. Mashtaka yote yalitokana na watuhumiwa kuandaa kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko, 2013 kama ifuatavyo:
1.   Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa Mh. Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P. Slaa;
2.   Kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi vya majungu kwa kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao wa Ushindi’ nje ya utaratibu wa Chama ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa;
3.   Kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na bila kupitia vikao halali vya Chama;
4.   Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini na ukanda vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii;
5.   Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;
6.   Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa Mwongozo wa Chama;
7.   Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania uongozi ndani ya Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
8.   Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
9.   Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa Chama;
10.                Kukashifu Chama na viongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge; na
11.                Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge.
UTETEZI WA WATUHUMIWA
Watuhumiwa wote walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya utetezi huo wa maandishi, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliitikia wito wa Kamati Kuu wa kujitetea kwa mdomo mbele yake. Hata hivyo, siku ya utetezi wao, ni Dr. Kitila Mkumbo peke yake aliyejitokeza kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa mdomo. Katika utetezi wake wa maandishi, licha ya kukiri kushiriki katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, Dr. Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa Samson Mwigamba – alikanusha na kukataa tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama, Kanuni zake na Mwongozo wa Chama. Kwa maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo alikanusha “kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi ya[ke]”, na kwamba mashtaka hayo sio ya kweli na hakuvunja Katiba, Kanuni wala Mwongozo wa Chama.
Aidha, licha ya kukiri kwake katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana kwamba walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni pamoja na mtu anayejulikana kama M2, mara hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia Kamati Kuu kwamba “waraka husika ulikuwa ni wa siri na haukuwahi kusambazwa wala kushirikisha … wanachama au viongozi wa CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Samson Mwigamba….” Vile vile, ijapokuwa katika Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana Dr. Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa M2, mara hii aliiambia Kamati Kuu kwamba anamfahamu fika M2 lakini hayuko tayari kumtaja mbele ya Kamati Kuu hadi atakapowasiliana naye!
USHIRIKI WA ZITTO ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA MABADILIKO
Itakumbukwa kwamba katika kikao cha Novemba 2013, Dr. Kitila Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe walikataa kata kata kuhusika kwa Zitto Zuberi Kabwe katika maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko. Aidha, Zitto Zuberi Kabwe alidai mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia Mkakati huo kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara nyingi na hadharani tangu avuliwe nafasi zake za uongozi. Hata hivyo, wakati wa mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila Mkumbo alikiri kwamba yeye na waandishi wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi Kabwe briefing juu ya Mkakati na kwamba alikuwa anaufahamu. Ukweli huu pia umethibitishwa na mawasiliano ya baruapepe iliyotumwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba, 2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Novemba iliyowavua madaraka.
Zaidi ya hayo, baada ya kuonyeshwa waraka wa Chama juu ya mabadiliko ya Katiba ya Chama uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama wakati huo Shaibu Akwilombe Julai 2006 unaothibitisha kwamba mabadiliko ya Katiba yaliyoondoa ukomo wa uongozi yalifanywa kwa uwazi na kwa kushirikisha ngazi zote za Chama, Dr. Kitila Mkumbo alikataa kata kata kujadili suala hilo kwa madai kwamba tayari walishapeleka malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Kuhusu tuhuma zao kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu wa fedha za Chama unaofanywa na Mwenyekiti wa Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha Anthony Komu na kwamba taarifa za matumizi ya fedha ni siri ya viongozi hao watatu, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa mbali mbali za fedha zilizowasilishwa mbele ya vikao vya Kamati Kuu a Chama ambavyo yeye mwenyewe na Zitto Zuberi Kabwe walishiriki kama wajumbe wa Kamati Kuu. Aidha, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa za kibenki zinazoonyesha jinsi michango ya Mzee Jaffer Sabodo na michango mingine ya watu binafsi zilivyopokelewa na kutumiwa na taarifa zake kuwasilishwa kwenye vikao vya Kamati Kuu walivyohudhuria yeye na Zitto Zuberi Kabwe.
Zaidi ya hayo, Dr. Mkumbo alionyeshwa nyaraka za manunuzi ya vifaa vya Chama kama vile vile pikipiki, kadi, bendera, n.k, na jinsi ambavyo uamuzi wa manunuzi hayo yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao wenyewe ni wajumbe na walihudhuria vikao husika. Vile vile, Dr. Mkumbo alionyeshwa ushahidi wa maandishi kwamba Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa namna yoyote ile katika manunuzi hayo na hakuna karatasi yoyote inayoonyesha saini ya Mwenyekiti katika manunuzi ya vifaa hivyo. Aidha, Dr. Mkumbo hakuweza kuthibitisha kwa namna yoyote kwamba CHADEMA ina mkataba wowote na watu binafsi wanaouza vifaa vya uenezi vya Chama kwa vile Kamati Kuu ya Chama katika vikao ambavyo vilihudhuriwa na Dr. Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe ilikwisharuhusu wafanya biashara binafsi kuagiza vifaa hivyo na kuviuza kwa wanachama wanaotaka kuvinunua. Kwenye yote haya, Dr. Kitila Mkumbo hakuwa na lolote la maana la kuiambia Kamati Kuu.
MAAMUZI YA KAMATI KUU
Baada ya kusikiliza utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na baada ya kumhoji kwa kirefu, Kamati Kuu imeridhika bila mashaka yoyote kwamba Mkakati wa Mabadiliko 2013 haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama peke yake. Mkakati huo ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa Chama kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi. Hii ni kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu, Chama cha siasa ambacho viongozi wake wa juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi kuaminiwa na wananchi kama tumaini lao la ukombozi.
Kamati Kuu imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali mbali zilizoandaliwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake wakitumia vitambulisho bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa kukibomoa Chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu. Mkakati huo ulihusisha pia hujuma dhidi ya Chama kwa kuwaengua wagombea wake katika chaguzi mbali mbali kama ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida Mjini ambapo Zitto Zuberi Kabwe alishiriki moja kwa moja.
Kwa sababu zote hizo, Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo:
1.    Kwamba kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wafukuzwe uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); na
2.    Kwamba, kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki Chama kinyume na matakwa ya Katiba ya Chama na Kanuni zake, na kwa vile Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya Chama visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe, viongozi wa ngazi zote za Chama, wanachama, washabiki na wapenzi wa CHADEMA popote walipo katika nchi yetu na nje ya Tanzania wasishiriki wala kusaidia kwa namna yoyote mikutano yoyote ya nje au ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto Zuberi Kabwe na mawakala wake kwa jina la CHADEMA.
——————————–
Dr. Wilbrod P. Slaa
KATIBU MKUU

0 comments:

Post a Comment