EAC (EAST AFRICA COMMUNITY) KUKUA KIUCHUMI BAADA YA KUWA NA SAFARU MOJA

Tuesday, December 17, 2013



Wengi wanaitazama hatua iliyochukuliwa na viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kuridhia kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja ni sawa na kusukuma tofali kwenye kina kirefu cha maji bila kuwa na matarajio ya kulifikia tena tofali hilo.
Kwa mujibu wa malengo ya jumuiya hiyo, kufikia mwaka 2023 mataifa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakuwa yamefikia shabaha ya kuwa na sarafu moja hatua ambayo itafungua uwanja mpya wa ushirikiano wenye nguzo tatu.
Kukamilika kwa shabaha hiyo kutategemea pia utashi wa kisiasa kutoka kwa nchi wanachama bila kujali idadi ya raia wake.
Iwapo shabaha hiyo itafanikiwa kama ilivyopangwa basi Kanda ya Afrika Mashariki itakuwa imeingia kwenye rekodi mpya kwa kuwa itakuwa Jumuiya ya pili kuwa na sarafu moja ya fedha ikitanguliwa na ile ya Umoja wa Ulaya.
Juhudi kama hizo za kuwa na safaru za pamoja zimewahi kufanywa na nchi zilizoko kwenye ushirikiano wa kibiashara kwa nchi za Asia ya mbali, lakini hazikuzaa matunda.
Mkataba wa Umoja wa Ulaya unaojulikana kama ‘Maastricht Treaty’ ulisainiwa kwa mara ya kwanza Februari 7, mwaka 1992 na baada ya kupita mwaka mmoja utekelezaji wake ulianza kazi. Umoja huu ulitimiza miaka mingine saba kutimiza ndoto ya sarafu moja ‘euro’.
Kwa kuzingatia biashara ya kubadilishana fedha na mtiririko wa biashara katika masoko ya kimataifa, sarafu ya euro inatajwa kuwa ni miongoni mwa sarafu zilipata mafanikio makubwa kwa kipindi kifupi baada ya kuanzishwa. Inasadikika baadaye huenda sarafu hiyo ikawa na nguvu katika soko la kimataifa.
Maktaba
Mkataba wa kuanzishwa kwa sarafu moja kwa nchi za Afrika Mashariki umesiniwa ikiwa imepita miaka 21 tangu kuasisiwa kwa mkataba wa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya. Pamoja na hatua hiyo iliyoanzishwa na viongozi wa Afrika Mashariki inatazamwa ikiwa ni sawa na kutosa tofali kwenye kina kirefu, lakini wanauchumi wanaona kwamba ni wazo linalokaribiana na ukweli.
Mbali na hayo kugundulika kwa rasilimali ghafi katika baadhi ya mataifa, ni moja ya vigezo vinavyofanikisha ndoto ya kuwa na sarafu moja. Kimsingi sarafu ya pamoja inaziwajibisha nchi wanchama kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kudhibiti kuporomoka kwa uchumi.
Eneo la Afrika Mashariki ambalo linakadiriwa kuwa na idadi ya watu wanaofikia milioni 135 lina uwezo wa kuzalisha bidhaa zitakazohimili ushindani wa kimataifa. Tanzania pekee ambayo kwa sasa ipo kwenye hatua za mwisho za kuchimba gesi na mafuta ina uwezo wa kuvutia wawekezaji wa moja kwa moja na kuzika kasumba ya miaka mingi ya utegemezi wa misaada kutoka mataifa yenye nguvu ya kigeni.
Iwapo mradi unaozinduliwa na Kenya wa ujenzi wa reli kwa msaada wa Serikali ya China utakamilika kwa wakati, mafuta yaliyogunduliwa hivi karibuni nchini Uganda na Kenya-utavutia wawekezaji wengi wa kigeni na kutoa msukumo mpya wa kibiashara miongoni mwa nchi wanachama. Reli hiyo itapitia katika baadhi ya nchi wanachama.

0 comments:

Post a Comment