Balaa tena! Watu 40 wahofiwa kufukiwa baada ya jengo la ghorofa 15 kuporomoka Dar

Friday, March 29, 2013

Dar es Salaam. Watu zaidi ya 40 wanahofiwa kufukiwa na kifusi baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa kuporomoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam jana asubuhi. Kuporomoka kwa ghorofa hilo lililokuwa katika Mtaa wa Indira Gandhi, kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea. Shughuli mbalimbali katikati ya jiji hilo zilisimama kwa siku nzima baada ya jengo hilo kuanguka na kusababisha vifo vya watu watano, 13 kuokolewa huku zaidi ya watu 40 wakisadikiwa kufukiwa na kifusi cha udongo wa jengo hilo. Jengo lililoporomoka Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida. Pamoja na vifo na wengine kujeruhiwa, magari takribani manne yalifunikwa na kifusi cha jengo hilo na kupondwa pondwa na kuwa kama chapati. Katibu wa Msikiti wa huo wa Shia Ithnasheri, Mushtaq Damji alisema: “Leo tulikuwa na kitu kama jumuiya kwa jamii ya wahindu, tulipanga kusherehekea lakini yote yakafutika. “Baada ya swala ya alfajiri, watu walikuwa wanazungumza hapa na pale na baada ya kupambazuka, watoto walikuwa wanacheza mpira, walikuwa 9. Sasa, bahati nzuri watoto saba wakakimbia na watoto wawili wakawa wamekwama,” alisema Damji.

0 comments:

Post a Comment