FAMILIA ya msanii Hussein Ramadhani Mkiety (Sharo Milionea) aliyekufa katika ajali wilayani Muheza wiki iliyopita imedai kuwa haiamini kwamba kifo cha mtoto huyo kilitokana na ajali, hivyo kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli. Mjomba wa marehemu , Mohamed Msenga alisema jana kwamba familia imekuwa na shaka juu ya mazingira ya kifo hicho baada ya kurejeshewa nguo za msanii huyo zilizokuwa zimeibwa baada ya ajali lakini hazikuwa na damu. Msenga alisema muda mfupi baada ya mama mzazi wa Marehemu Zaina Mwaimu Mkiety (54), kuitwa polisi na kukabidhiwa vitu mbalimbali zikiwamo nguo ambazo marehemu alikuwa amevaa siku ya ajali hawakuona hata alama ya damu jambo ambalo liliwashangaza. Alisema shaka hiyo ilianzia katika eneo ambalo ajali hiyo ilitokea akisema walipofika na kuonyeshwa mahala alipokuwa ameangukia, hawakuona damu jambo ambalo liliwatia shaka. Alisema begi la nguo za msanii huyo lilikuwa na udongo mwingi likionyesha kwamba walioiba walikuwa wamelifukia kabla ya kusalimisha lakini hakuna damu zilizoonekana. Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Teule Muheza, Dk Julius Mjema aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sharo Milionea alisema sababu ya kifo chake ni kichwa kupondeka. “Mimi ndiye niliyefanyia ‘postmoterm’ (uchunguzi), mwili wa Sharo Milionea, ni kwamba kichwa kilikuwa kimepondeka huku mifupa ya kichwa ikiwa imepondeka pia,” alisema Dk Mjema. Kuhusu madai ya nguo kutokuwa na damu, alisema marehemu alipata mpasuko wa ndani kwa ndani na siyo wa nje, ndiyo maana alipofikishwa chumba cha maiti damu zilionekana zikiwa zimeganda masikioni. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alipoulizwa kuhusu madai hayo ya familia alisema: “Hiyo ni taarifa ambayo jeshi la polisi litaifanyia kazi kwa kuingia kwa kina katika kuchunguza ili kuridhisha pande zote.” Mama yake alia kukosa mjukuu Katika hatua nyingine, mama mzazi wa msanii huyo amesema kutoachiwa mjukuu na tarehe za mwisho wa mwezi ni alama ambazo zitasababisha awe akimkumbuka mwanaye huyo milele. Akizungumza nyumbani kwake, katika Kitongoji cha Jibandeni Kijiji cha Lusanga wilayani hapa alisema kila ulipokuwa ukifikia mwisho wa mwezi ulikuwa ni muda wake wa neema kwani Sharo Milionea alimtumia fedha za matumizi yake binafsi pamoja na familia nzima nyumbani hapo. “Pamoja na kwamba kila mara alikuwa akinitumia fedha za kutatua shida zangu mbalimbali nilizokuwa nikimweleza lakini kila mwisho wa mwezi alikuwa akihakikisha anatuma fungu la matumizi yangu na ndugu zake hapa nyumbani,” alisema mama huyo. Alisema mwisho wa mwezi itakuwa ni alama ya kudumu ya kumbukumbu ya mwanawe kwa sababu ni wakati ambao alikuwa akimtumia fedha za matumizi yake pamoja na familia nzima. Kuhusu mjukuu alisema: “Sharo ni mwanangu wa pekee wa kiume, amekufa bila kuniachia mjukuu.. hii inaniuma sana lakini namshukuru Mungu kwani amechukua kiumbe chake na ndiye ajuaye siri iliyofichika mbele yangu,” alisema. Alisema hadi alipofariki hakuwahi kumdokeza juu ya kuwa na mtoto wala kumpa mimba msichana yeyote... “Unajua Sharo Milionea alizaliwa pacha na mwenzake Hassan lakini mwenzake alifariki dunia siku tano baada ya kuzaliwa kwa hiyo katika kizazi changu mwanangu pekee wa kiume alikuwa Sharo Milionea ambaye nilitumaini kwamba angeniletea wajukuu,” alisema Zaina. Alisema Sharo Milionea amekufa kabla hajatekeleza ndoto yake ya kumjengea nyumba ya kisasa pamoja na kuweka miradi ya kuboresha maisha yake azma ambayo aliiweka mwezi mmoja kabla ya kupata ajali iliyotoa uhai wake. Atoa ya moyoni kwa walioshiriki msiba Zaina alitoa shukrani za pekee kwa Rais Jakaya Kikwete na mkewe, Salma kwa kutuma ujumbe maalumu pamoja na rambirambi kutokana na msiba wa mwanaye huyo. Pia alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, wasanii, waandishi wa habari na kampuni mbalimbali zilizoshiriki pamoja na kutuma salamu za rambirambi.
Popular Posts
-
NEW YORK, Marekani VIDEO iliyoonyweshwa mwishoni mwa wiki katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ambayo ilielezea madhara ya taratibu ana...
-
RAIS Jakaya Kikwete ameeleza mikakati ya Serikali yake kuwa ni kuhakikisha inamaliza kabisa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ifikapo...
-
Uingereza imesitisha kwa muda msaada iliyokuwa iipe Rwanda kwa sababu ya wasiwasi kuhusu kuhusika kwa nchi hiyo katika mzozo uliopo Jam...
-
Huduma ya Maji na Nishati (EWURA), Mhandisi Godwin Samwel, akizungumza na wanahabari jana jijini, Dar es Salaam kuhusu kupanda kwa bei za m...
-
KAMPUNI ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti imetoa msaada wa kilo 200 ...
-
HERIETH MAKWETTA MSANII wa muziki wa kizazi kipya kutoka Tanzania, Rehema Chalamila maarufu kama Ray C, yupo katika kituo maalumu cha msa...
-
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewasafisha aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Ofisa Utawala wa ubalozi ...
-
UPELELEZI wa kesi inayomkabili Msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya mauaji katika Maha...
-
Wananchi wameshauriwa kutekeleza agizo la Utalii kwa wote kwa kuyatembelea maeneo mbali mbali ya utalii Zanzibar ili kufahamu historia y...
-
KUTOKANA na kile kichoonekana ni kutaka kukabiliana na uhaba wa sukari na kupanda kwa bei yake, Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatarajia kukuta...
Habari Leo Tanzania, Media, (East Africa)
0 comments:
Post a Comment