JOSEPH KABILA
Ni kijana na anawakilisha mustakabali wa nchi," Ndivyo walivyosema wafuasi wa Joseph Kabila wakati akiwasilisha fomu ya kugombea urais kwa muhula wa pili mwezi Septemba.
Akiwa na miaka 40, rais huyo anayetetea kiti chake ndio mgombea mwenye umri mdogo zaidi, ingawa tayari amekaa madarakani kwa miaka 10.
Alikuwa kamanda aiye na makuu katika jeshi, wakati baba yake Laurent-Desire Kabila alipouawa mwaka 2001, na aliteuliwa na watu wa karibu na utawala wa baba yake kuongoza DRC wakati huo ikitikiswa na mizozo mbalimbali ya wapiganaji.
Baadaye mwaka 2006 Bw Kabila alipata ushindi katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa kidemokrasia tangu uhuru.
Rais Kabila anaungwa mkono zaidi katika eneo la mashariki ambapo ndio alikozaliwa.
Alipata uungwaji mkono kidogo sana kutoka kwa wapiga kura wa upande wa magharibi katika uchaguzi wa mwaka 2006, huku wanaharakati wengi wa upande wa upinzani wakimtuhumu, bila ushahidi wowote, kuwa ni mzaliwa wa nchi jirani ya Rwanda, nchi ambayo imeivamia mara mbili DRC.
Bw Kabila alikulia nchini Tanzania na anazungumza Kiswahili na Kiingereza vizuri zaidi kuliko lugha zinazozungumzwa zaidi mjini KInshasa, yaani Kilingala na Kifaransa, lugha ambazo alilazimika kujifunza akiwa madarakani.
Kwa muda mwingi akiwa madarakani amekuwa kimya, akivunja ukimya huo tu wakati akizindua kampeni yake ya uchaguzi kwa kufanya mkutano na waandishi wa habari kwa muda wa saa tatu.
"Hatutapoteza uchaguzi huu. Nina uhakika na watu wetu, wameshuhudia jitihada na kujitolea," alisema.
Kampeni ya Bw Kabila ina msemo usemao "Maeneo matano ya ujenzi katika jamhuri", akiwa na maana ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya nchi, hasa ujenzi wa barabara na vituo vya nishati.
Lakini wananchi wengi wa Kongo wanalalamika kuwa kasi ya maendeleo ya kijamii ni ndogo mno.
Rais Kabila amekiri kuwepo kwa jambo hilo, akisema ana deni la kulipa kwa wapiga kura wa DRC na anawataka wamchague tena ili apate nafasi ya kulipa deni hilo.
Mr.ETIENE
Akiwa na umri wa miaka 79, Bw Etienne Tshisekedi, ndio mgombea mwenye umri mkubwa zaidi. Alizaliwa katika mkoa wa Kasai ya Kati mwezi Disemba mwaka 1932.
Alisomea sheria wakati wa utawala wa ukoloni wa Ubelgiji. Aliingia katika siasa wakati DRC ikipata uhuru mwaka 1960, ambapo alianza kwa kupata nyadhifa mbalimbali za ngazi ya juu serikalini, na pia katika utawala uliodumu kwa muda mfupi wa Kasai.
Alikuwa waziri wakati wa utawala wa kidikteta wa Mobutu Sese Seko, na alihamia upande wa upinzani mwaka 1980 wakati Bw Mobutu alipoamua kufuta uchaguzi wote.
Akiwa kiongozi wa chama cha UDPS, Bw Tsisekedi amekuwa mpinzani wa serikali mbalimbali tangu wakati huo.
Wakati Mobutu alipolazimishwa kuipeleka serikali yake katika mfumo wa vyama vingi mapema miaka ya 1990, Bw Tshisekedi alikuwa waziri mkuu mara mbili katika kipindi cha miaka miwili.
Aliondoka madarakani mara hizo mbili kutokana na mivutano mikali na Mobutu.
Chama cha Bw Tshisekedi hakikubeba silaha wakati wa mfululizo wa vita zilizosababisha kuanguka kwa utawala wa Mobutu mwaka 1997, na hivyo kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wananchi waliokuwa wameghubikwa na miaka mingi ya vita.
Baada ya kususia uchaguzi wa mwaka 2006, ambao alidai ulivurugwa mapema, Bw Tshisekedi ameahidi kushiriki kikamilifu safari hii na kupata ushindi.
Kwa baadhi ya watu, amevuka mipaka kwa kujitangaza kuwa ni rais kabla hata ya upigaji kura.
"Wananchi wa Kongo ni watu huru nchini humu na wamenitangaza mimi kuwa rais siku nyingi zilizopita," alisema wakati akizindua kampeni yake Novemba 11.
Wakosoaji wake wanasema matamshi kama hayo yanaweza kuchochea ghasia, hasa iwapo kama atapoteza uchaguzi.
Kukosekana kwake kwa mara kwa mara nchini humo kumeleta minon'gono kuhusu afya yake.
Bw Tshisekedi anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa katika eneo analotoka la Kasai na ia Kinshasa.
Wafuasi wake na wale wa Bw Kabila wamefarakana kwa misingi ya kikabila katika maeneo ya kusini mwa DRC, ambapo watu wengi kutoka Kasai wamehamia huko.
Chama cha UDPS kimekita mizizi yake na umaarufu upande wa kusini, lakini sio maeneo mengine nchini humo.
VITAL KAMERHE
Vital Kamerhe, 52, aliwahi kuwa mshirika wa rais Kabila, lakini sasa yuko upande wa upinzani.
Akiwa mmoja wa waasisi wa chama cha PPRD cha Kabila, Bw Kamerhe aliongoza kampeni za urais mwaka 2006 za Kabila.
Baadaye alikuwa spika wa bunge, hadi alipozozana na rais kuhusiana na makubaliano ya siri na rais ya kuruhusu Rwanda kupeleka wanajeshi wake mashariki mwa nchi kuwasaka waasi mapema mwaka 2009.
Bw Kamerhe ni mzaliwa wa upande wa mashariki katika mkoa wa Kivu, na aliojitoa serikalini na kuanzisha chama chake cha UNC.
Vital Kamerhe ni mwanasiasa na msomi anayezungumza vyema Kifaransa na Kiingereza, pamoja na lugha rasmi nne za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Anajiuza kwa wapiga kura wake -- kama mfano kwa kujifananisha na rais wa zamani wa Brazil Ignacio Lula da Silva.
"Nina uhakika kuwa eneo letu kijiografia na rasilimali, DRC kwa sasa ni kama tembo aliyelala, na ataamka kama Brazil," alisema.
Mtindo wake wa kufanya kampeni ni wa kiubunifu, akifanya mikutano katika maeneo wanaoishi watu maskini na kufanya mihadhara ya majadiliano ambapo watu wanakuwa huru kumuuliza maswali moja kwa moja.
Lakini wafuasi wengi wa upinzani bado wanamuona kama mtu aliye karibu sana na Bw Kabila, na ni mmoja wa wagombea 10 wanaotaka kuchukua kura kutoka kwa rais.
0 comments:
Post a Comment