Mawaziri wane wa JK Wangolewa na Bunge.
Dar es Salaam / Dodoma. Ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na
Mazingira iliyowasilishwa jana asubuhi bungeni mjini Dodoma, imewang’oa
madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilishindwa kusimamia vizuri utekelezaji
wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni
jana usiku na Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete
ametengua uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini
Marekani kwa matibabu.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya
kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa
Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai
Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo.
Waziri wa kwanza kutangaza kujiuzulu
alikuwa ni Kagasheki huku uamuzi wa mawaziri watatu kujiuzulu ukitangazwa na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kagasheki alitangaza kujivua wadhifa huo sa
2:09 usiku alipokuwa akichangia majumuisho ya ripoti ya kamati hiyo
iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo James Lembeli ambaye ni Mbunge wa
Kahama (CCM).
Katika maelezo yake Kagasheki alisema: “…Mimi
ni mtu mzima nimesikia hisia nzito sana kwa waliyoyasema wabunge. Rais
Kikwete aliponiteua ilikuwa ni kwa furaha yake na operesheni hii, yaliyotokea
yametokea hali ya wanyama huko si nzuri;
Mimi mwenyewe nimewasikia na nachukua fursa
hii kuteremka ngazi hii ya uwaziri na nitachukua taratibu za kawaida kuijulisha
sehemu inayohusika(Rais).
Baada ya Kagasheki kutangaza hatua hiyo, Spika
aliwaita mawaziri Dk Nchimbi na Nahodha kuchangia hoja hiyo, hata hivyo
hawakuwepo ndipo alipoitwa Dk Mathayo na kutoa maelezo yake.
Katika maelezo yake Dk Mathayo alisema kuwa
ripoti hiyo haikumtendea haki kwani kamati ya Lembeli haikumwita kumhoji na
kwamba hata ripoti nzima haikueleza kuhusika na kashfa hiyo. Hata hivyo
akihitimisha hoja hiyo Lembeli alisema Dk Mathayo ameshindwa kusimamia
mapendekezo tisa, yakiwemo matatizo ya wafugaji aliyopewa na
Rais Jakaya Kikwete Januari 18, 2006 alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Akitoa maelezo ya kutenguliwa kwa uteuzi wa
mawaziri hao, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Niliona nimtafute mkuu wa nchi (Rais
Jakaya Kikwete), nilimpa picha yote ya kinachoendelea, alikubali ushauri wa
Bunge; ..amekubali kuchukua ya uamuzi wa kutengua uteuzi wao(mawaziri).”
Akihitimisha mjadala huo wa ripoti ya kamati
yake, Lembeli alisema: “...Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara ya Maliasili na
Utalii nao wawajibishwe kutokana na kuhusika kwao na unyama uliotokea kwenye
mpango wa Operesheni Tokomeza Ujangili. Rushwa iliyopo ndani ya wizara hiyo ni
kubwa inakusanywa kwa kutumia simu, hivyo Serikali izichunguze simu zao kuanzia
leo.
Kizimbani kwa kuoa wanafunzi wawili ndugu
Kizimbani kwa kuoa wanafunzi wawili ndugu
JESHI la Polisi Wilaya ya Nkasi,
linamshikilia Pius Jacob, mkazi wa Kijiji cha Chala kwa kosa la kuoa mwanafunzi
wa darasa la tano katika shule ya msingi Kabwe, wilayani Nkasi.
Mtuhumiwa huyo pia anadaiwa kumuoa
dada wa mwanafunzi huyo ambaye ana miaka 16.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa
Dawati la Jinsia Nkasi, CPL-Anna Kisimba, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa
baada ya majirani kutoa taarifa polisi kuwa mtuhumiwa anaishi kinyumba na
wanafunzi hao.
Alibainisha kuwa mtuhumiwa huyo
alikamatwa baada ya kumchukua kwa nguvu binti huyo wa darasa la tano mwenye
umri miaka 12, na kwenda kuishi naye kama mke na mume.
“Tulikuwa katika ziara zetu za kawaida
zilizoambatana na siku 16 za kupinga ukatili tukizunguka baadhi ya vijiji vya
wilaya yetu, ndipo raia wema walituarifu kuwepo kwa tukio hilo na kuanza
kufuatilia hatimaye kumkamata mtuhumiwa,” alisema Kisimba.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo
ameshafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa Desemba 10
mwaka huu kwa kosa la kumuoa mwanafunzi na kubaka.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wa
Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye, alisema baada ya kufuatilia zaidi
waligundua mke wa kwanza wa mtuhumiwa huyo pia ni mwanafunzi ambaye hata hivyo
hakubainisha ni wa shule gani.
Mdenye, alisema majirani waliwaeleza
kuwa mtuhumiwa alimpata mwanafunzi wa pili kwa kutumia nguvu na vitisho.
“Hadi polisi na Ofisi ya Ustawi wa
Jamii tunafikiwa na taarifa hizo inadaiwa mtuhumiwa huyu alikuwa tayari ameishi
na binti huyu wa pili kwa wiki nzima nyumbani kwake, na majirani walijua baada
ya binti huyo kulalamika kwao kuwa alikuwa amechukuliwa kwa nguvu na
kulazimishwa kuolewa,” alisema Mdenye.
Matukio ya ukatili yanayoripotiwa
polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nkasi yamekuwa yakipungua
ambapo mwaka 2012 kulikuwa na kesi 224 za ukatili zilizoripotiwa ilhali kwa
mwaka 2013 ni kesi 143 tu ndizo zilizoripotiwa.
0 comments:
Post a Comment