Mwanamfalme Charles kuzuru Tanzania

Saturday, October 15, 2011


Mwanamfalme wa Uingereza Charles na mkewe Camilla, au The Prince of Wales and The Duchess of Cornwall, kama wanavyojulikana rasmi, watafanya ziara ya kiserikali Tanzania na Afrika Kusini mwanzoni mwa mwezi ujao kwa mwaliko wa serikali za nchi hizo mbili za kiafrika.Taarifa kutoka ubalozi wa Uingereza iliyotolewa Alhamisi inaeleza kuwa familia hiyo ya kifalme itazuru Tanzania kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika iliyokuwa ikitawaliwa na dola ya Uingereza.
Taarifa imeeleza kuwa ziara hiyo ni utekelezwaji wa mwaliko uliotolewa na rais Jakaya Kikwete, vile vile rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
“Serikali ya Uingereza imewaomba Prince of Wales na Duchess of Cornwall kufanya ziara rasmi nchini Afrika Kusini na Tanzania kuanzia Novemba 2 mpaka 9, kwa mwaliko wa Rais Zuma na Rais Kikwete”, imefafanua taarifa hiyo.
Majukumu
Ingawa hakuna maelezo ya kina wakiwa Tanzania watafanya shughuli zipi, inaamika kuwa pamoja na kukutana na Rais Kikwete, pia watatembelea kijiji kimoja cha jamii ya Masai, mbuga za wanyama kaskazini mwa Tanzania na pia wataenda visiwani Zanzibar.
Ziara yao nchini Tanzania itajikita katika maswala kama mahusiano ya kibiashara baina ya pande hizo mbili na uwekezaji; kuchochea upatikanaji wa ajira na maendeleo kwa ujumla vile vile utoaji wa fursa za elimu.
Wawili hao wajulikanao rasmi kwa lugha ya kimombo kama The Prince of Wales and The Duchess of Cornwall pia watazuru Afrika Kusini wakiwa wametokea Kuwait na Qatar.
Hii itakuwa ziara ya kwanza kwa Prince Charles tangu alipofika Tanzania mwaka 1984, alipozindua ujenzi wa barabara ya Makambako – Songea ambayo mpaka leo ni mhimili mkubwa wa usafirishaji kwenda mikoa ya kusini mwa Tanzania; ingawa mkewe hajawahi kuzuru kikazi nchi yoyote ya Kusini mwa Afrika.

0 comments:

Post a Comment