Brazil kuisaidia Tanzania kuendeleza sekta ya Kilimo

Monday, October 24, 2011


Serikali ya BRAZIL imekubali kuisaidia Tanzania katika sekta ya kilimo kwa kuwapa mafunzo wataalam wa kilimo na mifugo pamoja na kuwawezesha wakulima kupata zana bora ikiwa ni utekelezaji wa mpango maalum wa upatikanaji wa chakula barani Afrika ulioanzishwa na nchi hiyo.

Ahadi ya serikali ya Brazili imetolewa na waziri wa maendeleo vijijini wa nchi hiyo mjini Brasilia bwana Afonso Florence alipofanya mazungumzo na Waziri

Mkuu Mizengo Pinda ambaye amemweleza kuwa kikwazo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya kilimo ni teknolojia duni inayotumiwa na wakulima wa Tanzania na ukosefu wa wataalam.

Awali akisoma taarifa ya kilimo, Waziri Mkuu Pinda alimwarifu Waziri Afonso kuwa, licha ya Tanzania kujaliwa ardhi nzuri yenye rutuba ,wananchi wake wameweza kutumia asilimia 24 pekee ya ardhi yote huku matrekta yakitumiwa kwa asilimia kumi kiasi ambacho ni kidogo katika zama za sayansi na teknolojia.

Waziri Pinda pia ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa Brazil kuwekeza kwenye sekta ya kilimo nchini Tanzania ili kutoa mchango wao katika ukuaji wa uchumi na kuinua kipato cha wakulima.

Kesho Waziri Mkuu na ujumbe wake atatembelea kituo cha utafiti wa mazao kilichopo Brasilia.

0 comments:

Post a Comment