VYAMA vya CCM na Chadema vipo kwenye maandalizi ya mchakato wa kutafuta muafaka wa mgogoro wa umeya mkoa wa Arusha, baada Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa kuviandika barua ya kuvitaka viteue wajumbe wa kuunda kamati ya usuluhishi.
Hii itakuwa mara ya pili kwa CCM kukaa mezani na chama cha siasa cha upinzani kutafuta suluhu baada ya mtafaruku uliosababisha wananchi kuandamana na kutokea umwagaji damu.
Januari 2001, CUF iliongoza maandamano visiwani Zanzibar kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais wa visiwa hivyo, uliofanyika mwaka 2000 na kusababisha watu zaidi ya 20 kufa katika makabiliano ya polisi na waandamanaji ambapo risasi za moto zilitumika.
Januari, mwaka huu Chadema waliandamana kupinga namna uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji hilo. Katika kuzuia maandamano hayo, polisi wakabiliana nao, kwakutumia risasi za moto na kusababisha watu watatu kupoteza maisha.
Uchunguzi uliofanwa na gazeti hili
umegundua kuwa Tendwa amewaandikia barua viongozi wa vyama hivyo kuwaagiza kuwa wateue wajumbe watakaounda kamati maalumu itakayoshughulikia suala hilo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alithibitishia gazeti hili kuwa wamepata barua hiyo
Kwa mujibu wa barua ya Msajili yenye kumbukumbu namba CDM.112/123/01/17 ya Agosti 16, mwaka huu, ambaye Mwananchi Jumapili imeiona, vyama hivyo vimejulishwa juu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wa kuwepo timu ya pamoja kujadili na kuutafutia ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo.
Barua ya msajili iliyoandikwa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama na Dk Slaa wa Chadema zilipokelewa katika ofisi za vyama hivyo Agosti 17, mwaka huu.
Hata hivyo, juhudi za Mwananchi Jumapili kumpata Tendwa kwa njia ya simu zilishindikana kutokana na simu yake mkononi kutopatikana.
Barua ya Chadema yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/MSJ/04/65 ya Agosti 17, mwaka huu, pamoja na mambo mengine inakiri kuwa uundwaji wa kamati maalumu kutafuta muafaka wa mgogoro huo ulikuwa kiini cha
mazungumzo na makubaliano kati ya mwenyekiti wao, Freeman Mbowe na
Waziri Mkuu Pinda.
“Nakiri kupokea barua yako ya Agosti 16, mwaka huu. Nakiri pia kuwa huo ulikuwa msingi wa mazungumzo na mheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwenyekiti wa Chadema tarehe 6 Agosti, 2011.
"Chadema imekuwa ikisisitiza kuwa msingi
wa mgogoro huo ni ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi wa Meya...,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo iliyosainiwa na Dk Slaa inasema Chadema inapendekeza majadiliano na makubaliano yatakayofikiwa na kamati ya vyama hivyo iweke misingi wa kuondoa migogoro kama hiyo inayoweza kujitokeza
katika halmashauri nyingine za miji, Manispaa na majiji nchini.
Nakala ya barua hiyo yenye kurasa mbili imetumwa pia kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye Mwenyekiti wa taifa wa CCM, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman, Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika.
Kutokana na taarifa hiyo ya Tendwa, Chadema tayari imeteua wajumbe wanane wataongozwa na Dk Slaa katika vikao vya majadiliano na wenzao kutoka CCM.
Kwa mujibu wa barua hiyo, wengine katika timu hiyo ni wajumbe wa kamati kuu, Mabere Marando, Tundu Lissu na Lazaro Massay ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu na mwenyekiti wa mameya
na wenyeviti wa halmashauri zinazoongozwa na Chadema.
Wajumbe wengine ni Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, Mkurugenzi wa Halmashauri na Bunge, John Mrema, katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa na Diwani wa Kata ya Levolosi ambaye pekee ndiye
hakusaini muafaka uliosababisha wenzake kutimuliwa, Ephata Nanyaro.
Dk Slaa alikiri kupokea barua ya msajili iliyowajulisha uwepo wa kamati vya vyama hivyo kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa umeya Arusha na kuteua wajumbe watakaoshiriki kutoka chama chake.
Hata hivyo, Dk Slaa hakuwa tayari kuzungumzia msimamo wa chama chake na matarajio yao, hasa baada ya Waziri Mkuchika kuagiza madiwani waliofukuzwa kuendelea kushikilia nyadhifa zao na kupewa
stahiki zote za udiwani na halmashauri ya Arusha.
Mkuchika aliagiza wiki hii madiwani hao wapewe haki hizo ikiwa ni pamoja na posho zao hadi mahakama itakapotoa uamuzi juu ya kesi ya kupinga kufukuzwa kwao uanachama na chama chao.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nnape Nnauye, alikataa kuzungumzia suala hilo akisema kuwa hayo ni majungu.“Hayo ni majungu,” alisema Nnauye alipotaka kujua kama Tendwa amethibitisha kwa kinywa chake kuhusu muafaka huo.
Nnauye ambaye amekuwa mmoja wa viongozi wa CCM walio mstari wa mbele kukisafisha chama chake dhidi ya viongozi wenye kashfa za kifisadi, alisema atakuwa tayari kujibu hoja iliyotoka moja kwa moja kinywani mwa Tendwa na siyo maandishi.
Tendwa hakuweza kupatikana kuzungumzia mpango huo baada ya kutafutwa kwa muda mrefu kupitia simu yake ya mkononi bila mafanikio.
Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni hivi karibuni, Waziri Mkuu aliwaruka viongozi wa Chadema waliokuwa wameeleza kuwa kamati ya usuluhishi katika mgogoro wa Arusha itaundwa na kwamba, viongozi wa chama hicho na Pinda walishakubaliana.
Pinda alikiri kukutaa na viongozi Slaa na Mbowe lakini aliwaambia kuwa jukumu la kuunda kamati ya kuratibu mwafaka Arusha litafanywa na Tendwa kwa vile yeye hana mamlaka hayo.
Kauli hiyo ilimfanya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) kuomba mwongozo wa Spika na kusema Waziri Mkuu alilidanganya Bunge kwa vile alikubaliana na viongozi wa Chadema juu ya suala hilo.
0 comments:
Post a Comment