Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Libya akamatwa

Saturday, September 24, 2011


Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Libya Al-Baghdadi al-Mahmoudi, amekamatwa nchini Tunisia.
Kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa Tunisia Bw Mahmoudi alikamatwa Jumatano jioni kusini mwa Tunisia karibu na mpaka wa Algeria.

Bw Mahmoudi alihudumu kama Waziri Mkuu hadi pale Kanali Gaddafi alipong'olewa mamlakani mwezi jana.
Kanali Gaddafi bado hajulikani alipo wakati huu ambapo wafuasi wake bado wanashikilia ngome zao chache ambazo zimezingirwa na vikosi vya utawala mpya.

Taarifa moja ya televisheni inayosimamiwa na baraza la mpito la kitaifa NTC imesema kuwa Bw Mahmoudi alikuwa amezuiliwa katika eneo la Tamaghza karibu na mpaka wa Tunisia na Algeria.
Amekuwa akijaribu kuvuka mpaka lakini amejisalimisha bila matatizo.

Taarifa hiyo inasema kuwa alikuwa na hati bandia.

Algeria imekuwa na uhusiano mbaya na utawala mpya wa Libya na pia ilimpa hifadhi mke wa Gaddafi na wanawe watatu.
Lakini hii leo shirika rasmi la habari la Algeria limesema Wizara ya mashauri ya kigeni ya Algeria imesema iko tayari kufanya kazi kwa karibu na utawala huo mpya wa Libya.

Televisheni ya Al-Arabiya imemnukuu Waziri wa mashauri ya kigeni wa Algeria akisema nchi yake imejiunga na nchi nyengine katika kulitambua rasmi baraza la NTC kama mtawala mpya wa Libya.

Wakati huohuo nchini Libya,vikosi vya NTC vimesema vimekamata miji yote mitatu mikubwa katika eneo la chemichemi la al-Jufra kusini mwa nchi hiyo.

0 comments:

Post a Comment