Jeshi la Muungano wa Afrika katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, linasema wanamgambo wa kundi la Kiislam la Al-Shabab baado ni tishio, na AU inahitaji wanajeshi zaidi elfu tatu kudumisha usalama mjini humo.
Wakati AU ikihitaji wanajeshi hao wa ziada, suali kubwa ni kwa nini nchi za Kiafrika zilizoahidi kutuma wanajeshi zinasita kujiunga na operesheni hiyo ya kulinda amani.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2007, operesheni ya kulinda amani ya Muungano wa Afrika nchini Somalia imekuwa ikipigania kupata askari wa kutosha wanaohitajika kuisaidia serikali dhaifu ya mpito katika mji mkuu, Mogadishu.
Wakati ikianzishwa, AMISOM, ilihitaji wanajeshi elfu nane.
Nchi wanachama wa Muungano wa Afrika zilitoa ahadi ya kutuma wanajeshi, lakini ahadi hizo hazijawahi kutekelezwa.
Ni mataifa ya Uganda na Burundi pekee, ambayo hadi sasa wako na askari wao katika mistari ya vita mjini Mogadishu.
Nchi hizo mbili sasa zinajiandaa kutuma kutuma wanajeshi wa ziada elfu tatu.
Hata hivyo, kulingana na msemaji wa AU, El Ghassim - wane, Djibouti nayo kwa sasa iko tayari kutuma wanajeshi 850 mwezi October, pamoja na wakufunzi mia moja wa kijeshi.
Sierra Leone iliahidi kutuma kikosi miaka michache iliyopita.Lakini kwa wakati huu inajiandaa kufanya tathmini , kabla ya uamuzi rasmi wa kuwatuma wanajeshi wake, labda mwaka ujao.
Ghana, Nigeria Cameroon, Mali, Senegal, Zambia na Malawi ni baadhi ya nchi ambazo pia ziliwahi kutoa ahadi ya kutuma vikosi vyao.
Kuna sababu kadhaa zinazofanya baadhi ya nchi kujizuwia kutuma wanajeshi katika nchi kama Somalia, ambayo imekuwa na machafuko na kutokuwa na serikali kuu kwa zaidi ya miongo miwili.
Mataifa mengine, yasingependa kuona wanajeshi wao wakirudishwa nyumbani katika majeneza.
Kuna pia suala la kutoaminia. Kuna taarifa zisemazo wanajeshi wa serikali ya mpito na wale wa Muungano wa Afrika hawaaminiani.
Pia kuna madai ya ukosefu wa mshikamano, uwajibikaji na uratibu bora katika serikali inayolega lega ya mpito ya Somalia, ambayo hadi mwishoni mwa juma lililopita ilikuwa inadhibiti sehemu ndogo kabisa ya mji mkuu.
Lakini msemaji wa AU El-Ghassim Wane amekanusha madai yote haya
0 comments:
Post a Comment