MBUNGE APINGA NAFASI ZA DRC

Wednesday, December 5, 2012

MBUNGE wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu, ameungana na wananchi wanaotaka Katiba Mpya ifute uwepo wa wakuu wa wilaya na mikoa kwa madai kuwa viongozi hao wamewekwa kisiasa zaidi na siyo viongozi wa kiserikali kama inavyodhaniwa hivi sasa. Sugu alitoa mapendekezo hao wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Saza wilayani Chunya mkoani Mbeya kwenye mkutano wa hadhara ambapo alisema kuwa, Katiba ijayo ifute cheo hicho kwani kipo kwa ajili ya kutetea masilahi ya chama tawala na siyo kusimamia rasilimali za Serikali na wananchi wake. Alisema kuwa wakuu wa wilaya na mikoa wangekuwa wapo kama wawakilishi na watendaji wa Serikali kama wanavyodhani walio wengi wasinge kuwa wanashiriki katika shughuli za kisiasa kwani hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi(CCM), wakati kikifanya chaguzi za chama hicho viongozi hao pia walikuwa mstari wa mbele katika shughuli za chama hicho. “Ndugu zangu wananchi wa kijiji cha Saza, nasema hivi naungana na wananchi wote waliojitokeza na kutoa maoni yao kwa tume ya kuratibu na kukusanya maoni na kupendekeza kuwa cheo cha mkuu wa mkoa na wilaya kifutwe kwani hawa watu wapo kwa maslahi ya kutetea chama tawala na si vinginevyo,” alisema. Alisema kuwa viongozi hao kwa kuwa hawatambui kazi yao wala nafasi yao ina umuhimu gani kwa wananchi ndiyo maana inafika mahala wanajifanyia mambo watakavyo na kubwa zaidi ni kuendelea kukumbatia shughuli za chama tawala. Mbunge huyo alisema kuwa katika ngazi ya wilaya, shughuli zote zinafanywa na kusimamia na mkurugenzi mtendaji mkuu huku ngazi ya mkoa shughuli zote zinafanywa na kusimamiwa na Katibu tawala wa mkoa hivyo ukiangalia nafasi ya mkuu wa wilaya na mkoa hawana kazi yoyote maalumu.

0 comments:

Post a Comment