Nchi kubwa na yenye rasilimali nyingi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) imekuwa katika kile kinachotajwa kuwa vita vya Dunia vya Afrika. Hali hiyo imeaicha nchi katika janga la kuhitaji misaada ya kibinaadamu.
Mapigano ya miaka mitano yalitikisa serikali, ikiungwa mkono na Angola, Namibia na Zimbabwe, dhidi ya waasi wanaoungwa mkono na Uganda na Rwanda.
Licha ya mpango wa amani na kuundwa kwa serikali ya mpito mwaka 2003, watu upande wa mashariki mwa nchi hiyo wamesalia kuwa katika hali ya wasiwasi kutokana na kuwepo kwa makundi ya wanamgambo na wanajeshi yanayowasumbua.
Vita hivyo vilisababisha vifo vya takriban watu milioni tatu, ama kutokana na mapigano ya moja kwa moja au kutokana na magonjwa na utapia mlo. Hali hiyo imetajwa kuwa huenda ndio baa kubwa kuwahi kutokea barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni.
Vita hivyo vilikuwa na athari za kiuchumi na za kisiasa. Mapigano yalichochewa na hazina kubwa ya utajiri wa madini, huku pande zote mbili zikitumia mwanya huo kufuja rasilimali. Historia ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imekuwa na sura mbili, moja ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na ya ufisadi. Baada ya uhuru mwaka 1960, nchi hiyo mara moja ilikabiliwa na jeshi kufanya mgomo na jaribio la kutaka kujitenga kwa jimbo lenye utajiri wa madini la Katanga.
Mwaka mmoja baabaye, waziri mkuu wa wakati huo Patrice Lumumba alikamatwa na kuuawa na wanajeshi wanaomtii mkuu wa majeshi Joseph Mobutu.
Mwaka 1965 Mobutu alichukua madaraka, na baadaye kuibadili jina nchi hiyo na kuiita Zaire na yeye kujiita Mobutu Sese Seko. Aliigeuza Zaire kuwa eneo la harakati dhidi ya Angola iliyokuwa ikiungwa mkono na Jamhuri ya Kisovieti na hivyo yeye kupata kuungwa mkono na Marekani. Lakini pia aliidumbukiza Zaire katika ufisadi.
Baada ya vita baridi, Zaire ilipoteza umuhimu wake kwa Marekani. Hivyo, mwaka 1997, wakati nchi jirani ya Rwanda ilipovamia Zaire kuwasaka wanamgambo wa Kihutu, iliwapa nafasi waasi wanaompinga Mobutu ambao mara moja waliuteka mji wa Kinshasa na Laurent Kabila kuingia madarakani na kuwa rais na kulirejesha jina la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Hata hivyo, matatizo ya DRC yaliendelea. Mzozo kati ya Bw Kabila na washirika wake wa zamani ulianzisha uasi mwingine, uliokuwa ukiungwa mkono na Rwanda na Uganda. Angola, Namibia na Zimbabwe zikachukua upande wa Kabila na hivyo kuigeuza nchi hiyo kuwa uwanja wa vita.
Majaribio ya kupindua serikali na ghasia za hapa na pale ziliendelea kurindima na kuanzisha mapigano mapya mashariki mwa nchi hiyo mwaka 2008. Wanamgambo wa Kihutu kutoka Rwanda walipambana na wanajeshi wa serikali mwezi Aprili na kusababisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao.
Kundi jingine la waasi chini ya Jenerali Laurent Nkunda lilitia saini makubaliano ya amani mwezi Januari, lakini mapigano yalizuka tena mwezi Agosti. Majeshi ya Jenerali Nkunda yalisonga mbele na kuingia katika ngome za serikali na mji wa GOma na kusababisha raia na wanajeshi kukimbia huku majeshi ya kulinda usalama ya Umoja wa Mataifa kujaribu kushikilia maeneo pamoja na wanajeshi waliosalia wa serikali.
Katika jaribio la kuleta hali ya utulivu, serikali mwezi Januari mwaka 2009 ilialika wanajeshi kutoka Rwanda kusaidia kuwasaka waasi wa Kihutu wanaofanya shughuli zao mashariki mwa DRC.
Rwanda ilimkamata hasimu mkuu wa waasi wa Kihutu, Jenerali Nkunda, ambaye ni Mtutsi aliyeonekana kama mpinzani mkuu katika eneo hilo.
Hata hivyo, mwaka 2009, ulisalia kuwa na hali ya wasiwasi katika maeneo ya mashariki.
0 comments:
Post a Comment