MAWAZILI MIZIGO WAITESA CCM

Tuesday, December 17, 2013






*Nape asema kuwatimua kunaweza kusiwe na tija
Hatma ya mawaziri saba wanaotajwa kuwa ni mizigo sasa ipo mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, baada ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi(CCM) kuwahoji juzi.

Hata hivyo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema kuwa kumfukuza Waziri inaweza isiwe tija kwa sababu matatizo yanayosababisha wizara zao kulalamikiwa yanaweza kuwa ni ya kisheria au kimfumo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nape alisema baada ya Kamati Kuu kuwahoji mawaziri hao, ilitoa ushauri kwa Mwenyekiti wa chama hicho ambaye ni Rais Jakaya Kikwete.

Ingawa Nape hakusema ni ushauri gani walioutoa lakini alisisitiza kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye mwenye dhamana ya kuteua au kuwaondoa mawaziri.

“Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi(CC) iliwahoji mawaziri saba jana(juzi), kuhusu madai mbalimbali ambayo wizara zao zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi...tulisikiliza utetezi wao na baada ya mahojiano tulitoa ushauri wetu kwa Mwenyekiti ambaye ndiye mteuzi wao,” alisema.

Aliwataja mawaziri hao waliohojiwa kuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais , Utumishi, Celina Kombani. 

Wengine ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Naibu Waziri wa Fedha Saada Salum Mkuya, Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Dk. Mathayo David pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Abdallah Kigoda.

Akifafanua hoja ya kutimuliwa kwa mawaziri mizigo, Nnape alisema kazi ya Kamati Kuu(CC) ni kumshauri mwenyekiti wa chama kwamba yeye ndiye aliyepokea ushauri wao hivyo jukumu la kuwafukuza, kuwabakisha au kuwabadili wizara lipo mikononi mwake.

“Ukiniuliza kwamba Kamati Kuu ilimshauri nini mwenyekiti, nitakuwa kama nashinikiza maamuzi maamuzi ya mwenyekiti, kikubwa ni kwamba yeye ndiye mwenye kuufanyia kazi ushauri tuliompa,” alisema Nnape.

Aidha aliongeza kuwa kumfukuza Waziri inaweza isiwe tija kwa sababu matatizo yanayosababisha wizara zao kulalamikiwa yanaweza kuwa ni ya kisheria au kimfumo.

“Tusikimbilie kutimua watu tu, kunamambo ya kuangalia kwa mapana zaidi kwenye baadhi ya wizara... mifumo na sheria zibadilishwe ili kuendana na mazingira,” alisema Nnape.

Katika hatua nyingine alisema Kamati Kuu imeshauri mambo mbalimbali kwa serikali ambayo yanatakiwa yafanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.

Miongoni mwa ushauri huo ni pamoja na kulipa madeni ya walimu ambayo yanadaiwa kwa muda mrefu pamoja na kuweka mfumo bora kwa kuzuia kuzaliwa kwa madeni mapya.

Ushauri mwingine ni kulipa madeni ya wakulima wa mahindi pamoja na kuweka mpango maalumu wa kuhakikisha Korosho zinabanguliwa ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa.

“Katika hoja hii serikali ikome kabisa kukopa mazao kwa wananchi...katika ziara ya siku 26 tulioimaliza hivi karibuni, tulipofika mkoa wa Ruvuma tulikuta malalamiko haya kwamba serikali imekopa mahindi kwa wakulima na imepita miezi sita hawajalipwa, swali la kujiuliza baada ya kulipigia kelele suala hili fedha zimepatikana, hivi zilikuwa wapi fedha hizi?” alihoji Nnape.

Akiendelea kusoma ushauri huo wa CC kwa serikali, alisema wakulima wasilazimishwe kutumia mbolea za minjingu hivyo kupendekeza kwamba wakulima wapewe uhuru wa kutumia mbolea ya aina yoyote.

Pia serikali iweke mfumo madhubuti kwa ajili ya kilimo cha mkataba kwa kutoa uhuru zaidi kwa wakulima wa mazao.

Aidha CC imeishauri serikali kuweka mkakati wa kupunguza urasimu hasa kwenye utoaji wa vibari vya wawekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.

Ushauri mwingine kwa serikali ni kuweka mfumo bora wa uendeshaji wa vyama vya ushirika nchini

Kwa upande wa utekelezaji wa Ilani ya CCM, Nape alisema sekta ya miundombinu imefanya vizuri huku akipongeza juhudi za wananchi kwa kushirikiana na serikali katika ujenzi wa maabara, nyumba za walimu pamoja na nyumba za madaktari

0 comments:

Post a Comment